OTHMAN ASISISTIZA KUWA SERIKALI YA UMOJA NI MUHIMU KWA AMANI
MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ametoa mwito kwa wananchi waiunge mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kulinda amani na utulivu.
Othman alisema hayo katika kikao na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa Bililo Malindi Unguja jana.
Alisema licha ya uwepo wa changamoto ya baadhi ya watu kupinga kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa wananchi wanapaswa kuiunga mkono ili kuwa na umoja, amani na utulivu.
“Wanaopinga haya wana sababu zao siyo za nchi, sisi tunaamini nchi yetu ina fursa ya kwenda mbali sana tukiwaleta watu pamoja tukafanya kazi pamoja, mimi ninaamini na ninawajua watu ambao wapo ndani ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) wazuri, hodari na waadilifu,” alisema
Aliongeza: “Nawaomba kwa dhati kabisa sisi wote tuna dhamana, sisi tumefika hapa tumemeza makubwa… Ni lazima tufaidike na nchi yetu, uislamu wetu, mwenendo wetu , malezi, utukufu wa nchi yetu, kwa kuendesha mambo yetu kwa salama, tuwaunganishe watu pamoja hasa”.
Othman alisema ushirikiano wa wananchi walioutoa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025 umewezesha wananchi kuwa na amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi huo.
Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu walikutana na serikali na kukubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Othman alisema walikubaliana mambo saba likiwemo la kurejesha imani kwa wananchi kwa kuwa na tamko la pamoja la kutekeleza ajenda hiyo.
Alisema pia walikubaliana kuunda tume huru ya uchaguzi itakayosimamia masuala ya uchaguzi kuwa huru na haki na kuanza kwa mchakato wa kutungwa katiba mpya.
Makubaliano mengine ni kufanya mageuzi ndani ya mfumo wa haki, utumishi wa umma na kuwepo wa Kitambulisho cha Mzanzibar na kuundwa kwa tume ya maridhiano.
Othman alisema makubaliano hayo yatawezesha kufanya tathimini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuhusu namna inavyoweza kufanywa ikawa bora kwa maslahi ya wananchi na kuweka mfumo wa utekelezaji na kuunda ratiba ya utekelezajaji huo.
Alisema kwa sasa itaundwa tume ya pamoja itakayohusisha wajumbe wa pande zote za serikali ya umoja wa kitaifa ili kushauri na kuweka utaratibu na utekelezaji wa makubalianao pamoja kuwepo kwa tume ya kusimamia utekelezaji.
Kwa mujibu wa Othman, makubaliano ya kuunda umoja huo ni kwa ajili ya mustakabali wa vizazi vijavyo kwa kutafuta suluhu ya nchi na kuweka kando maslahi ya watu binafsi.
“Leo tuliopo sote tunajua nchi yetu ilipotoka na inapokwenda hawa tunaowaona wanaokuja baada ya sisi hatuoni watakuwa na faida tuliyonayo sisi, hatudhani kama atatokea Karume (Abeid Aman Karume) au Shein (Ali Mohamed Shein) wala Othman (Othaman Masoud Othman) mwingine, sisi tuna dhamana, tuitazame nchi yetu, tusitafute suluhu ya vyama yetu, tutafute suluhu ya nchi yetu,” alisema.

Post a Comment