MTIKISIKO NA KISHINDO CHA TAMASHA LA KIZIMKAZI




Shamrashamra za Tamasha la Kizimkazi Festival leo lipo katika kilele chake huku Rais Samia Suluhu Hassan n akiongoza maelfu ya wananchi na wageni kutoka sehemu mbalimbali kushiriki matukio muhimu katika ukanda wa Kizimkazi, Unguja.

Kwa leo katika tamasha hili  kubwa la kiutamaduni na kimaendeleo lililoanza Agosti 12, 2026, leo tarehe 13 Agosti 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana shiriki ratiba nzito na yenye shughuli mbalimbali za uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika ukanda wa Kizimkazi.

Katika nyakati za asubuhi, Mheshimiwa Rais anatarajiwa kupanda mti katika Hospitali ya Kizimkazi na kukabidhiwa magari yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Baada ya hapo, atafanya ziara ya kutembelea chanzo cha maji katika eneo la Pango la Machomwe. Aidha, Mheshimiwa Rais ataendelea na shughuli za kuweka jiwe la msingi na kupanda mti katika Chuo cha Amali VETA Kizimkazi kilichopo Kibuteni.

Majira ya mchana, Mheshimiwa Rais atafanya ufunguzi rasmi wa tangi la maji na kupata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi wa Kizimkazi ili kusikiliza kero zao na kutoa maelekezo ya serikali.

Shughuli za Rais zitahitimishwa kwa kishindo usiku wa leo katika "Usiku wa Kizimkazi Festival." 

Mheshimiwa Rais atahudhuria tamasha hilo kubwa litakalojumuisha burudani za aina mbalimbali zikiwemo vichekesho, Taarab asilia, ngoma za asilia, muziki wa dansi Bongo Fleva, na maonyesho ya wasanii wa All Stars. Tukio hili la usiku litafanyika katika Viwanja vya Suluhu Sport Academy.

Tamasha hili ambalo limekuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Kusini Unguja, linatarajiwa kuhitimishwa rasmi kesho, Agosti 14, 2026, katika Uwanja wa Mwehe uliopo Makunduchi, tukio litakalopambwa na uwepo wa viongozi wa juu wa kitaifa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kilele cha tamasha hilo kesho kinatarajiwa kuwa na msisimko wa kipekee ambapo wananchi watapata fursa ya kusikiliza nasaha za viongozi na kushuhudia hitimisho la miradi mbalimbali iliyokuwa ikitekelezwa kwa kipindi cha mwaka mzima. Tamasha hili limeendelea kuthibitisha kuwa si tu tukio la kijamii, bali ni jukwaa muhimu la kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii na uchumi wa buluu, likiimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi katika kuleta maendeleo endelevu.

No comments