Mkuu wa Wilaya ya Ilala Atua Kimanga na Kuahidi Huduma ya Uhakika ya maji



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameweka dhamana ya kuhakikisha wananchi wa Kata ya Kimanga, hasa Mtaa wa Darajani, wanapata huduma ya maji ya uhakika kupitia uboreshaji wa miundombinu iliyopo, ikiwemo kisima kinachozalisha lita 60,000 kwa saa na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000. 

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu uliokuwa ukiwasababishia adha kubwa hasa wanawake wanaolazimika kuamka usiku wa manane kutafuta maji. 

Katika ziara hiyo, amesisitiza kuwa miundombinu hiyo iliyopo inapaswa kutumiwa kikamilifu ili kusogeza huduma karibu na wananchi, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha ununuzi wa pampu mpya nane kutoka Mto Ruvu na kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, hatua inayothibitisha dhamira ya serikali ya kuondoa kero za wananchi.


No comments