Jihan Dimack Atawazwa Miss Grand Tanzania 2026 Katika Usiku Wa Kihistoria


Historia mpya katika ulimwengu wa urembo nchini Tanzania imewekwa, baada ya mrembo Jihan Dimack kutawazwa kuwa Miss Grand Tanzania 2026. 

Fainali hizo za kusisimua zimefanyika katika Ukumbi wa kifahari wa The Super Dome uliopo Masaki nakuhudhuriwa na umati mkubwa wa wapenda masuala ya urembo na urimbwende .

Jihan, anayebeba bendera ya Mkoa wa Mwanza, aliibuka mshindi baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha haiba, uwezo wa kujieleza, na mvuto wa kipekee katika hatua mbalimbali za shindano hilo—kuanzia vazi la kuogelea, vazi la jioni, hadi kipengele cha maswali magumu kutoka kwa majaji. 

Kwa ushindi huu, Jihan sasa anabeba jukumu zito la kuiwakilisha Tanzania katika mashindano makubwa ya kimataifa ya Miss Grand International yanayotarajiwa kufanyika nchini India.

Mafanikio ya Jihan hayakuja kwa bahati mbaya, kwani usiku huo wa fainali ulishuhudia ushindani mkali kutoka kwa warembo wengine mahiri walioingia katika hatua ya tano bora. 

Nafasi ya mshindi wa pili (First Runner Up) ilichukuliwa na mrembo kutoka Arusha, Prisca Lyimo, ambaye pia alitunukiwa taji la Miss Cosmo Tanzania 2026 na anatarajiwa kupeperusha bendera ya taifa nchini Vietnam. Mshindi wa tatu (Second Runner Up) alikuwa ni Celine Edson kutoka Mkoa wa Shinyanga, aliyetawazwa kuwa Miss Earth Tanzania 2026 na atashindana nchini Philippines. Orodha ya washindi wa juu imekamilishwa na Namala Patrick kutoka Geita, aliyetawazwa kuwa Miss Tourism Africa Tanzania 2026.

Tukio hilo la aina yake halikuwa na lengo la kumtafuta mshindi mkuu pekee, bali lilikuwa jukwaa la kutoa mataji makubwa manne ya kimataifa kwa wakati mmoja, jambo linaloashiria kuimarika kwa tasnia ya urembo nchini. 

Katika kuonyesha thamani ya ushindi huo, washindi wakuu watatu wa kwanza wamezawadiwa magari mapya aina ya Nissan Dualis, motisha ambayo haijawahi kushuhudiwa mara nyingi katika mashindano ya ndani na hivyo kuongeza chachu ya ushindani.

Msisimko wa usiku huo ulianza kushika kasi wakati wa hatua ya Top 14, ambapo warembo kutoka mikoa mbalimbali—ikiwemo Mtwara, Simiyu, Kigoma, Arusha, Shinyanga, Mwanza, Morogoro, Tabora, Geita, Songwe, Mbeya, Rukwa, Kilimanjaro, na Dar es Salaam—walifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuonyesha utayari na uwezo mkubwa. 

Hatua ya Evening Gown ilikuwa kilele cha kuonyesha umaridadi na ustadi wa kutembea jukwaani, huku mashabiki wakishuhudia mabadiliko makubwa ya hisia ukumbini wakati wa Final Walk ya malkia wa mwaka jana, wakiongozwa na Miss Grand Tanzania 2025, Beatrice Alex.


No comments