Dawa za kulevya ndizo zimemuua nyota wa NBA Brandon Clarke




Maafisa wa uchunguzi wa vifo vya ghafla mjini Los Angeles wameweka wazi kuwa nyota wa timu ya mpira wa kikapu ya Memphis Grizzlies, Brandon Clarke, alifariki dunia kutokana na athari za matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroini na kokeini. 

Ikiwa ni takriban miezi mitatu tangu alipofariki dunia Mei 11 mwaka huu,Ripoti rasmi kutoka kwa mchunguzi wa vifo hivyo imethibitisha kuwa kifo hicho cha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kilikuwa cha bahati mbaya. 

Siku hiyo ya tukio, kikosi cha zima moto na uokoaji kilijibu mwito wa dharura katika eneo la San Fernando Valley na kumkuta mchezaji huyo amefariki dunia nyumbani kwake, huku vyombo vya dola vikikuta vielelezo vya mihadarati eneo la tukio jambo lililofanya uchunguzi wa awali kucheleweshwa ili kufanya vipimo vya kina.

Wakati wa kifo chake, mchezaji huyo ambaye alichezea timu ya Grizzlies kwa misimu yake yote saba ya NBA na kukosa msimu wa 2025 hadi 2026 kutokana na majeraha, alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kuendesha gari kwa kasi na kumiliki dawa za kulevya kufuatia tukio la kukimbizana na polisi huko Arkansas mwezi Aprili. 

Uongozi wa timu ya Memphis Grizzlies ulionesha kushtushwa na msiba huo mzito ukimuelezea kama mchezaji bora na mtu mwema aliyetoa mchango mkubwa kwa jamii, huku wachezaji wenzake akiwemo Jaren Jackson Jr. wakielezea simanzi kubwa kwa kupoteza rafiki wa karibu ambaye walikuwa kama pacha, wakati dada wa marehemu, Taylor Triplett, akiwashukuru wananchi wote kwa upendo na salamu za pole walizozipata katika kipindi hiki kigumu.

No comments