DC Mpogolo Aongoza Operesheni Maalum ya Usafi Dar: Bilioni 3 Zatengwa Kurejesha Haiba ya Jiji



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameongoza zoezi kabambe la usafi wa mazingira kwenye maeneo mbalimbali wilayani humo, huku akisisitiza kuwa mkakati huo utakuwa endelevu na si wa msimu. 

Katika zoezi hilo, Mhe. Mpogolo ameambatana na viongozi waandamizi, akiwemo Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Sheria kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bw. Elibariki Bajuta, pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Ndg. Elihuruma Mabelya, ambapo kwa pamoja wameshiriki kusafisha eneo la Daraja la Salender.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa mvua zilizonyesha hivi karibuni zilisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo mengi ya Ilala. Kutokana na kukatika kwa mvua hizo, uongozi wa wilaya umejizatiti kufanya usafi wa kila siku ili kurejesha taswira ya kuvutia ya Jiji la Dar es Salaam, huku akitoa wito kwa wadau wa mazingira kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi hizo za serikali.







Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka NEMC, Bw. Elibariki Bajuta, ameahidi kutoa ushirikiano thabiti kwa Mkuu wa Wilaya ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote. Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu, hasa kuelekea maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ambapo wageni wengi wanatarajiwa kufika nchini na kutumia maeneo ya katikati ya jiji.

Katika kuongeza nguvu kwenye mkakati huo, Mkurugenzi wa Jiji, Elihuruma Mabelya, ametangaza kuwa Halmashauri imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 3 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/27 mahsusi kwa ajili ya uboreshaji na utunzaji wa mazingira.

Zoezi hili la usafi wa pamoja ni sehemu ya utaratibu endelevu uliowekwa na Mkuu wa Wilaya. Katika awamu hii, usafi huo umefanyika kwa mafanikio makubwa katika maeneo ya Daraja la Salender, pembezoni mwa uwanja unaojengwa wa mazoezi wa Gymkhana, pamoja na barabara kuu za katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

No comments