DC MPOGOLO AHIMIZA WANANCHI KUDUMISHA UTAMADUNI WA MAZOEZI



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewapongeza wanachama wa Unique Fitness Club pamoja na washiriki wa klabu mbalimbali za jogging walioshiriki maadhimisho ya miaka sita ya klabu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa mazoezi katika kuboresha afya za wananchi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mpogolo alisema mazoezi ya mara kwa mara yana mchango mkubwa katika kuimarisha afya na kuwahamasisha wananchi kuendelea kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha ya kila siku.

Maadhimisho hayo yaliwakutanisha washiriki kutoka klabu mbalimbali za jogging waliokusanyika kusherehekea mafanikio ya Unique Fitness Club tangu kuanzishwa kwake miaka sita iliyopita.






Katika hafla hiyo, washiriki walishiriki matembezi na mbio za pamoja, sambamba na shughuli mbalimbali zilizolenga kuhamasisha umuhimu wa mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

Kwa upande wao, viongozi wa Unique Fitness Club walisema kuwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita, klabu hiyo imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki mazoezi ya mwili pamoja na kukuza ushirikiano miongoni mwa wanajamii.

Aidha, baadhi ya washiriki waliohudhuria maadhimisho hayo walieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi, huku wakiahidi kuendelea kushiriki shughuli za mazoezi kwa lengo la kuboresha afya zao.

Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa wito wa kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi na kudumisha ushirikiano miongoni mwa wanajamii.

No comments