Hatimaye Koffi Olomide afunga ndoa na Cindy Le Coeur
Hatimaye, mfalme wa miondoko ya Ndombolo na kiongozi wa bendi ya Quartier Latin, Koffi Olomide (69), amevunja ukimya wa miaka mingi kwa kufunga ndoa rasmi na mwandani wake wa muda mrefu, mwanamuziki Cindy Le Coeur (43).
Tukio hilo la kukata na shoka, ambalo limewashtua na kuwafurahisha mashabiki kote ulimwenguni, lilifanyika Jumamosi, Februari 28, katika sherehe ya kiserikali iliyopambwa na anasa, mitindo, na mahaba mazito.
Baada ya kudumu kwenye uhusiano kwa takriban miongo miwili, wawili hao wameamua kuirasimisha safari yao mbele ya ofisa wa serikali na mashahidi wachache wa karibu.
Kama ilivyo ada ya "Grand Mopao," Koffi hakuangusha upande wa mavazi. Akiwa na umri wa miaka 69, alitokelezea kama mfalme wa kisasa akivalia suruali pana ya rangi ya maziwa (cream), koti lenye nakshi za dhahabu, na buti nyeupe zenye visigino Virefu.
Kwa upande wake, Cindy Le Coeur aling’ara kwa urembo uliopitiliza akivaa suruali ya rangi ya maziwa iliyoendana na blauzi ya pinki. "Sote tulikuwa warembo na tulipendeza, tuking’ara kama kawaida," aliandika Koffi kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akisindikiza na video za tukio hilo.
Moja ya matukio yaliyovuta hisia za wengi ni pale Koffi alipokuwa akimvisha pete Cindy. Gwiji huyo alionekana kunong’ona maneno fulani ya Kifaransa yaliyojaa ucheshi, jambo lililowafanya wahudhuriaji kuangua kicheko kabla ya wawili hao kupiga busu la dhati kuziba agano lao.
Jambo lingine la kipekee lilikuwa kitendo cha Koffi kusindikizwa madhabahuni na binti yake, Minou Olomide, ishara iliyoonyesha baraka za kifamilia katika ndoa hiyo ya kihistoria.
Kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wamefurika kutoa pongezi, wengi wakisifu uvumilivu wa Cindy ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa bendi ya Koffi kwa miaka mingi. "Hatimaye malkia amepata taji lake," aliandika shabiki mmoja, akirejelea safari ndefu ya wawili hao kuanzia jukwaani hadi kwenye ndoa.
Koffi alimalizia kwa ujumbe mfupi wa baraka kwa wafuasi wake: “Furaha yetu na iwe yenu.”

Post a Comment