VIJANA WANENA: MATUSI NA UDHALILISHAJI MTANDAONI SASA BASI
Kikundi cha Amani nchini kimeelezea kuchoshwa na wimbi la matusi, kashfa na udhalilishaji wa viongozi wa kitaifa unaofanywa na watu wanaojiita wanaharakati wa mitandaoni, huku kikihimiza hatua kali za kisheria kuchukuliwa mara moja.
Katika mkutano maalumu uliofanyika jijini Tanga, kikundi hicho kimeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kuwafuatilia na kuwatia mbaroni watu wanaotumia majukwaa ya kidijitali kupotosha ukweli na kuichafua taswira ya nchi.
Hatua hii inakuja wakati kukiwa na malalamiko kuwa baadhi ya watumiaji wa mitandao wameacha kuitumia kwa maendeleo na badala yake wameigeuza kuwa kichaka cha kupandikiza chuki na kudhoofisha juhudi za serikali.
Mjumbe wa kikundi hicho, Rehema Manyama, amebainisha kuwa katika kipindi kifupi cha siku mia moja tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan achaguliwe, ameweza kuonyesha uthubutu wa kipekee kwa kutekeleza ahadi zilizogusa maisha ya Watanzania wengi.
Mafanikio hayo ni pamoja na kuimarisha huduma za afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote, kutoa nafasi za kazi kwa vijana elfu kumi na mbili, na kuleta utulivu wa kisiasa nchini. Rais amepongezwa kwa kufungua milango ya diplomasia ya kimataifa na kutengeneza fursa mpya za kiuchumi ambazo sasa zinawapa vijana matumaini ya kujikwamua kimaisha badala ya kupoteza muda kwenye malumbano yasiyo na tija.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Amani, Hassan Kubebelwa, amewaasa vijana kuwa macho na watu wanaoshinda kwenye mitandao wakielezea mapungufu pekee na kuficha maendeleo makubwa ya miundombinu yanayotekelezwa nchi nzima.
Amesema ni wakati wa vijana kusimama kidete na kuelezea mazuri ya nchi yao badala ya kusikiliza upotoshaji unaolenga kuwavunja moyo. Amesisitiza kuwa serikali imetoa mabilioni ya fedha kupitia mikopo ya asilimia kumi kwenye halmashauri, hivyo vijana wanapaswa kuchangamkia fursa hizo kuanzisha miradi ya uzalishaji badala ya kukaa kijiweni na kulalamika mtandaoni.
Kwa upande wao, wajumbe wa kikundi hicho akiwemo Zuberi Gogo na Zainabu Salim Ugata, wamefafanua kuwa ingawa changamoto ndogo ndogo za kiutendaji haziwezi kukosekana, juhudi za makusudi zinafanyika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi bila upendeleo.
Wamefafanua kuwa mikopo ya asilimia kumi inatolewa kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa kila mwananchi mwenye sifa, na wamejipanga kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya uzalendo. Kikundi hicho kinaamini kuwa kupitia elimu ya amali na kujenga uelewa wa mambo ya serikali, vijana watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kuingiza kipato, jambo ambalo ndilo jibu sahihi kwa wale wanaojaribu kuwatumia kama daraja la kufanya fujo na udhalilishaji.

Post a Comment