MAPINDUZI YA KIDI JITALI TRA: JINSI UBUNIFU WA VIJANA UNAVYOKWENDA KUZIBA MIANYA YA KODI NA KUIMARISHA UCHUMI WA TAIFA




Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetikisa anga la teknolojia nchini baada ya kuwatangaza na kuwazawadia vijana wabunifu walioleta masuluhisho ya kidijitali yanayolenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. 

Hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam mnamo Februari 25, 2026, imethibitisha kuwa taasisi isiyokumbatia ubunifu hupitwa na wakati, huku vijana wa Kitanzania wakipewa rungu la kuongoza mapinduzi ya kiuchumi kupitia kiganja cha teknolojia.

Katika hali ya kusisimua, Bwana Gabriel Mashenene ameibuka mshindi wa kwanza kwa kupata wastani wa alama 92 na kujinyakulia kitita cha Shilingi milioni 50, ngao pamoja na cheti. Mashenene ameshinda kupitia wazo lake la kipekee la "KodiTrack", ambao ni mfumo wa Smart Invoice & Import Verification unaotumia teknolojia ya kidijitali kupambana na ankara bandia na udanganyifu wa uagizaji bidhaa. Mfumo huo unafanya uhakiki wa taarifa za mizigo kwa wakati halisi, hatua itakayosaidia kupunguza upotevu wa mapato na kupanua wigo wa kodi nchini.

Nafasi ya pili imeshikiliwa na Edmund Komba aliyepata alama 73 na kuzawadiwa Shilingi milioni 30 kwa ubunifu wake wa kutumia QR Code na GPS Tracking. Mfumo huu utawashirikisha wananchi moja kwa moja kuhakiki uhalali wa bidhaa na kutoa taarifa za papo kwa papo (Live Alerts) kwa TRA endapo watabaini bidhaa bandia au zisizolipiwa kodi. Ubunifu mwingine uliovutia wengi ni wa Emma Sambaya, aliyepata alama 72 na zawadi ya Shilingi milioni 30, baada ya kupendekeza kuunganishwa kwa stakabadhi za EFD na mfumo wa NHIF ili kila mlipakodi anapopata risiti, sehemu ya kodi hiyo ichangie bima yake ya afya na kumhamasisha kudai risiti.

Mamlaka hiyo pia imetambua nguvu ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) na Blockchain kupitia washindi wengine waliojinyakulia mamilioni ya fedha. Malehe Masubi alizawadiwa Shilingi milioni 30 kwa kutumia AI kurahisisha kazi zinazojirudia, huku Ismael Mkumbi akiondoka na Shilingi milioni 20 kwa mfumo wa SmartTax unaotumia Blockchain kuhifadhi taarifa za walipakodi kwa usalama. Washindi wengine waliojinyakulia Shilingi milioni 20 kila mmoja ni pamoja na Ng’wang’wa Loyani, Erick Joachim, Ajra Noordin Ismail, na Hubayb Said kwa mifumo inayolenga kurahisisha huduma za kodi kupitia simu na mitandao ya kijamii.

Akikabidhi tuzo hizo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameipongeza TRA kwa hatua hiyo akisema itasogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ushirikishwaji katika ukusanyaji wa kodi. Waziri amesisitiza kuwa jukumu la kodi ni la kila mwananchi, na hata wale ambao hawakushinda wamechangia katika kuimarisha nchi kwa kutoa mawazo yao. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bw. Uledi Mussa Abasi, aliongeza kuwa tuzo hizi ni mkakati wa kuifanya TRA iwe karibu zaidi na walipakodi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema kuwa tuzo hizo ni endelevu na dirisha la kupokea mawazo mapya kwa mwaka wa fedha 2025/2026 litafunguliwa kuanzia Aprili 1 hadi Juni 30, 2026.

Amesema kuwa kupitia ubunifu huo, TRA inatarajia kuboresha huduma na kuongeza wigo wa kodi, jambo ambalo linaweza kuleta matumaini ya kupungua kwa viwango vya kodi hapo baadaye kutokana na kuongezeka kwa makusanyo. Jumla ya mawazo 5,681 yaliwasilishwa na kuchujwa hadi kupatikana washindi tisa bora waliohitimisha mchakato huo.

No comments