MAAGIZO YA KIHONGOSI YANAONESHA TAIFA LINALODAI UWAJIBIKAJI
KATIKA hali inayozidi kuonesha kuwa CCM imedhamiria kusafisha urasimu na uzembe katika usimamizi wa rasilimali za umma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amemlipua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na madiwani wake.
Kihongosi ametoa agizo kali akitaka halmashauri hiyo kuacha mara moja matumizi ya fedha kwenye safari na mafunzo yasiyo na tija, badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye ununuzi wa madawati ili kukomesha adha ya wanafunzi kukaa chini.
Hatua hiyo imekuja Februari 20, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara ambapo wananchi walipaza sauti zao kulalamikia uhaba mkubwa wa samani katika shule zao.
Akizungumza kwa uchungu mbele ya mamia ya wananchi, Kihongosi amesisitiza kuwa utumishi wa viongozi hauna maana yoyote ikiwa watoto wa wapiga kura wanateseka kusoma katika mazingira magumu ilhali viongozi wao wanatumia fedha za walipa kodi kwa safari za anasa.
Amewataka viongozi wa halmashauri hiyo kuwa na roho ya ubinadamu na kuumizwa na kero za wananchi badala ya kujali maslahi yao binafsi. Kihongosi ameweka wazi kuwa ni jambo lisilokubalika kuona viongozi wakijificha kwenye kivuli cha mafunzo ya nje ya wilaya wakati darasani watoto hawana hata mahali pa kuandikia.
Sambamba na agizo hilo la kiutendaji, mjadala wa umma umezidi kupata mashiko kupitia kauli za wadau na wakazi wa maeneo mbalimbali nchini kuhusu umuhimu wa utulivu katika kuchochea maendeleo hayo.
Bi. Rahma Salum, mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam, ametoa rai nzito kwa vijana nchini akihimiza ulinzi wa amani kama msingi mkuu wa kila kitu. Kwa mujibu wa Bi. Rahma, amani ni utulivu ambao ukikosekana, hakuna shughuli yoyote ya kijamii wala kiuchumi inayoweza kufanyika, hivyo amewataka vijana kutojihusisha na chochezi za vurugu ili kuilinda Tanzania ambayo imekuwa mfano wa utulivu kwa miaka mingi.
Mchanganyiko wa maagizo ya Kihongosi na rai ya amani kutoka kwa wananchi unajenga picha ya taifa ambalo sasa linadai uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa viongozi wake huku likidumisha amani.
Ujumbe wa Kihongosi umekuwa onyo kwa viongozi wote nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitavumilia viongozi wanaoendekeza masilahi ya safari huku miradi ya msingi ya kijamii kama elimu ikisua. Ni matarajio ya wananchi wa Kasulu kuwa agizo hili litatekelezwa kwa kasi ya radi ili kurejesha heshima ya elimu katika wilaya hiyo na mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
Post a Comment