Falsafa ya Magufuli Kuangaziwa Katika Kitabu Kipya cha PAWA Nchini Guinea
Chama cha Waandishi wa Afrika (Pan African Writers Association – PAWA) kinatarajia kuzindua kitabu kinachomuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, katika Maonesho ya Vitabu ya Conakry yanayotarajiwa kufanyika Aprili 2026 nchini Guinea Conakry.
Kitabu hicho kimetolewa kama kumbukumbu ya maisha na uongozi wa Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, na kinakusanya mitazamo mbalimbali ya Waafrika kuhusu mchango wake katika siasa na maendeleo ya bara.
Kitabu hicho ni mkusanyiko wa mashairi na insha zilizoandikwa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili na waandishi 46 kutoka nchi 27 za Afrika pamoja na diaspora ya Kiafrika. Kimehaririwa na Rais wa PAWA, Profesa Bill Ndi wa Chuo Kikuu cha Tuskegee nchini Marekani, na ni kitabu cha tatu katika mfululizo wa machapisho ya PAWA yanayowaenzi viongozi mashuhuri wa Afrika. Vitabu vilivyotangulia vilimhusu aliyekuwa Rais wa Ghana John Jerry Rawlings na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi Profesa Wole Soyinka.
Kitabu hiki kinaangazia safari ya uongozi wa Magufuli kama kiongozi aliyesisitiza uwajibikaji, nidhamu na kujitegemea. Kauli mbiu yake maarufu “Hapa Kazi Tu” inaelezwa kama falsafa ya kujenga maendeleo yanayotegemea uwezo wa Waafrika wenyewe.
Kupitia mashairi na tafakuri za kitaaluma, kitabu kinamchora Magufuli kama kiongozi aliyepinga mazoea yaliyokuwepo na kuhimiza mwelekeo mpya wa maendeleo ya taifa na bara la Afrika. Uzinduzi wa Conakry utakuwa wa kwanza kabla ya matukio mengine yatakayofanyika katika nchi mbalimbali za Afrika baadaye mwaka huu.
Post a Comment