Dkt. Samia akizindua Kikombo asema: Hakuna Uchumi Imara Bila Ulinzi Madhubuti

 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahimiza Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuimarisha mshikamano wa kitaasisi, kulinda heshima ya Jeshi na kuepuka mienendo inayoweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa vyombo vya ulinzi. 

Aidha, amewataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu, uaminifu na dhamira ya dhati ya kulitumikia Taifa.

Rais Dkt. Samia pia amewataka Watanzania wote kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa ulinzi wa Taifa ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya dola.

Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyojengwa eneo la Kikombo, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.

Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa Kikombo unaashiria hatua mpya ya nchi katika safari ya kuimarisha mifumo ya ulinzi sambamba na kasi ya mageuzi ya kiuchumi, kijamii na taasisi yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. 

Rais Dkt. Samia amesema uwekezaji katika miundombinu ya ulinzi ni sehemu ya msingi ya kulinda heshima ya Taifa, amani ya nchi na mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi, akitaja kuwa kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa makao hayo ni matokeo ya mipango ya muda mrefu ya Serikali ya kujenga taasisi imara za kitaifa kwa kutumia rasilimali na wataalamu wa ndani.

"Makao Makuu haya ni alama ya ukomavu na uwezo wetu kama Taifa wa kupanga, kuamua na kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha na wataalamu wetu wa ndani," alisema Rais Dkt. Samia.










Akizungumzia mabadiliko ya mazingira ya kiusalama duniani na uwezo wa mamlaka za ulinzi kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutumia Makao Makuu hayo mapya kama kitovu cha uratibu wa kimkakati, uchambuzi wa kitaalamu na usimamizi wa kisasa wa shughuli za ulinzi wa Taifa.

"Mazingira ya kiusalama hayalindwi kwa silaha pekee, bali kwa taarifa, teknolojia, mifumo ya mawasiliano na mbinu za kisasa," alisisitiza.

Katika kuunganisha dhana ya ulinzi na maendeleo ya Taifa, Rais Dkt. Samia amesema ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaongeza wajibu wa Serikali na taasisi zake katika ulinzi wa rasilimali, miundombinu na uwekezaji unaofanyika nchini, na kuongeza kuwa hakuna Taifa linaloweza kudumisha ustawi wa wananchi wake bila kuwa na taasisi madhubuti za kulinda mipaka, rasilimali na watu wake.

"Serikali yetu itaendelea kuliwezesha Jeshi letu kuwa na mazingira bora ya kazi ili liwe tayari, wakati wote, kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi," alisema Rais Dkt. Samia, akisisitiza kuwa uwekezaji katika ulinzi ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa Taifa.

Rais Dkt. Samia ametoa pongezi kwa uongozi wa awamu zilizopita, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na JWTZ kwa mchango wao katika utekelezaji wa mradi huu katika hatua mbalimbali na kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itafanikisha ujenzi wa awamu zilizosalia ili kukamilisha taswira halisi ya Makao Makuu hayo ya kisasa.

No comments