CCT YAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KUJENGA MAHUSIANO
Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT) imepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza ari ya Mahusiano miongoni mwa jamii ya kitanzania hatua itakayosaidia kuleta utengamano na mshikamano wa kidugu.
Hatua hiyo imekuja kupitia kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alipokutana na Viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Februari 18, 2026 mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kufanya majadiliano yatakayosaidia kuandaa nyaraka za kuimarisha ushirikiano wa kitaifa.
Akizungumza kwenye kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa Pili wa CCT na Askofu Mkuu wa Kanisa La Mennonite Church Tanzania Askofu Nelson Kisare ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa kuona maono ya kuanzisha Wizara ambayo inasimamia Mahusiano na Misingi ya Mahusiano ni amani, upendo, maadili mema, uongozi unaojali haki na usawa kwa wote na hii ni namna nzuri ya kujenga mahusiano ya nchi kuwa pamoja na kurudisha uzalendo kwa vijana.
Waziri Sangu kwa upande wake alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefungua milango ya majadiliano na mazungumzo na taasisi za dini ili wadau kama viongozi wa dini waijue dira hii na watambue mipango kazi ya serikali kwenye kuyafikia maono ya taifa na kwamba Jumuiya hiyo (CCT) ni mdau muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Miaka 25 ijayo.
“Tumekutana kujadili namna ya kuimarisha mahusiano na kuendeleza ushirikiano. Msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa,” alisema Sangu.
Alisema CCT ni mdau ambae ameshirikiana na serikali kwa muda mrefu kupitia uratibu wa makongamano ya kidini, Muendelezo wa miradi ya Maendeleo ya Jamii, misaada kwa Kaya masikini na Ajira kwa watanzania.
Sangu alibainisha kuwa serikali inatambua kazi wanazofanya CCT kwa jamii na amewapongeza kuwa daraja la kuwaunganisha watanzania pamoja na serikali.
Waziri Sangu anaendelea na ziara za kukutana na kuzungumza na viongozi wa wadau wa sekta ya mahusiani wakiwemo madhehebu ya dini, asasi za kijamii, siasa na makundi ya vijana ili kutambulisha jukumu la wizara yake kuhusu ujenzi wa Mahusiano chanya yatakayosaidia kuchochea ustawi wa jamii.
Post a Comment