AFCON 2027: Sekta ya uchukuzi kuibeba Tanzania kimataifa



Tanzania inaingia katika ramani ya dunia ya michezo kwa kishindo, ikijipanga kutumia mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kama jukwaa la kuitangaza nchi na kukuza uchumi. 

Serikali kupitia Msemaji Mkuu, Gerson Msigwa imebainisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanamichezo na mashabiki wanapata usafiri wa uhakika na wa kiwango cha kimataifa. 

Amesema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha kwamba wanajitangaza kwa nguvu kupitia vyombo hivyo juu ya uwapo wa Afcon 2027 nchini Tanzania na nini cha kufanya kufurahisa uwapo wake.

Amesema kuongezeka kwa idadi ya ndege kufikia 16, zikiwemo za masafa marefu kama Boeing 787-8 Dreamliner, kutasaidia kuunganisha Tanzania na mataifa mengine kushiriki kwa urahisi zaidi.Kwa sasa ATCL imepanua mtandao wake wa safari hadi kufikia vituo 33, jambo ambalo litarahisisha harakati za timu na wageni mbalimbali. 

"Uwepo wa ndege hizi mpya na za kisasa unatoa picha ya nchi iliyojiandaa kutoa huduma bora za usafiri wa anga, jambo ambalo ni kigezo muhimu katika uendeshaji wa mashindano makubwa ya michezo. Serikali inalenga kutumia usafiri wa anga kama daraja la kuleta mataifa ya Afrika nchini Tanzania kwa ajili ya shamrashamra za soka" alisema  Msigwa akizungumza na waandishi wa habari Februari 26 mwaka huu.

Vilevile, uboreshaji wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini, vikiwemo viwanja vya kitalii kama Arusha na Kilimanjaro, unalenga kumpokea kila mgeni anayekuja kwa ajili ya michezo na utalii. Ujenzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) utasaidia kupokea viongozi wa mashirikisho ya soka na mataifa mbalimbali kwa heshima na hadhi ya kidiplomasia. Hii inaonyesha jinsi miundombinu ya uchukuzi inavyofanya kazi bega kwa bega na sekta ya michezo.

Mkakati wa "Sport Tourism" (Utalii wa Michezo) unapewa kipaumbele kikubwa, ambapo watalii wanaokuja kwa ajili ya AFCON wanahamasishwa kutembelea vivutio kama Hifadhi ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro. 

Kwa upande wa usalama, Serikali imehakikisha kuwa viwanja vyote vya ndege vimefungwa mashine za kisasa za ukaguzi ili kulinda usalama wa wageni wote msimu wa michezo. Hii inatoa imani kwa mashirikisho ya kimataifa kuwa Tanzania ni mahali salama kwa mashindano na shughuli za kijamii. 

Mafanikio ya kibiashara yanatarajiwa pia kupitia mauzo ya bidhaa za utamaduni na michezo kwa wageni watakaotumia usafiri wa reli ya SGR na ndege za ATCL. SGR itakuwa kiungo muhimu cha kuwasafirisha mashabiki kati ya miji mwenyeji wa mechi, ikipunguza muda wa safari na kuongeza msisimko wa mashindano. Hii ni mara ya kwanza kwa miundombinu ya kisasa kiasi hiki kutumika kuunga mkono sekta ya michezo nchini Tanzania.

"Kila kitu kipo sawa tunaomba watanzania wote kujibrand  kwa michuano hii na kuipa heshima stahiki kwa kuwa ni fursa" alisema Msigwa.

Msigwa amesisitiza kuwa uwekezaji huu wa siku 100 na mwendelezo wake ni sehemu ya maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya michezo kuwa sekta inayozalisha ajira na kuitangaza nchi. Kupitia AFCON, Tanzania inatarajia kuvuna matunda ya uwekezaji huu kwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha hadhi yake kimataifa. Hivyo, michezo sasa si burudani tu, bali ni uchumi wa kidijitali na miundombinu unaosonga mbele.


No comments