TIKTOK YAINGIA MITINI DAKIKA ZA MWISHO: Yakimbia Kesi ya "Uraibu" wa Mitandao
Mtandao maarufu wa kijamii wa TikTok umeamua kufanya suluhu ya siri na kukubali yaishe ili kuepuka kuingia kwenye mnyororo wa kesi ya kihistoria inayohusu athari za uraibu wa mitandao ya kijamii.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni saa chache tu kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuchagua baraza la wazee la mahakama (jury) kule California, Marekani, ambapo mtandao huo ulitakiwa kuanza kujitetea dhidi ya tuhuma nzito za kuharibu afya ya akili ya vijana.
Kesi hiyo imefunguliwa na binti mmoja mwenye umri wa miaka 20, aliyetambulika kwa herufi za KGM, ambaye anadai kuwa mfumo wa "algorithms" wa mitandao hiyo umeundwa kwa makusudi ili kumfanya mtumiaji awe mraibu (addicted).
Binti huyo anadai kuwa hali hiyo imempelekea kupata matatizo makubwa ya afya ya akili, ikiwemo sonona na matatizo ya ulaji. Ingawa masharti ya suluhu hiyo yamefanywa kuwa siri, kitendo cha TikTok kukubali yaishe kinaashiria hofu kubwa waliyonayo matajiri wa teknolojia dhidi ya nguvu ya sheria.
Sakata hili sasa limebaki kuwakabili wababe wengine wa mitandao akiwemo Meta, ambao ni wamiliki wa Instagram na Facebook, pamoja na kampuni ya Google inayomiliki mtandao wa YouTube. Mtandao wa Snapchat wenyewe ulishasalimu amri na kufanya suluhu wiki iliyopita. Kampuni hizi zimekuwa zikijitetea kwa miaka mingi kupitia sheria ya mwaka 1996 inayowalinda kutokana na kile kinachowekwa na watu wengine kwenye mitandao yao, lakini safari hii mambo yamebadilika kwani kesi hii inahusu jinsi mifumo yao ya ndani inavyowateka watumiaji kwa nguvu.
Wakili wa binti huyo, Matthew Bergman, ameliambia shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kuwa huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa kwani kampuni hizi sasa zitalazimika kueleza mbele ya mahakama kwa nini faida zao ni muhimu kuliko maisha na afya za vijana. Anasema kuwa kuna maelfu ya watoto ulimwenguni kote wanaoteseka kwa sababu ya mifumo hatari ya mitandao hiyo ambayo inawalazimisha watumiaji kubaki mtandaoni kwa muda mrefu bila kujitambua.
Moja ya matukio yanayosubiriwa kwa hamu kubwa ni ushahidi wa bosi wa Meta, Mark Zuckerberg, ambaye anatarajiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake. Zuckerberg amekuwa akishikilia msimamo kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaounganisha mitandao ya kijamii na matatizo ya afya ya akili kwa vijana, kauli ambayo inapingwa vikali na watafiti pamoja na familia nyingi zilizoathirika. Wataalamu wa sheria wanasema kuwa mabosi wa teknolojia mara nyingi hupoteza utulivu wanapokuwa chini ya shinikizo la maswali ya mawakili mahakamani.
Hali hii inatokea wakati ambapo nchi mbalimbali zinaanza kuchukua hatua kali kudhibiti mitandao hiyo. Kwa mfano, Australia tayari imepiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16, huku Uingereza ikionyesha nia ya kufuata nyayo hizo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa enzi za kampuni za teknolojia "kudekezwa" na sheria zimeanza kufika kikomo, na sasa ni wakati wa kuwajibika kwa madhara wanayosababisha katika jamii.

Post a Comment