TANZANIA NA FIFA KUIMARISHA USHIRIKIANO: FURSA ZAIDI KWA VIJANA KUFUNGULIWA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, ameeleza utayari wa shirikisho hilo kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza programu mbalimbali za maendeleo zitakazowanufaisha vijana nchini. 

Ushirikiano huo utajikita zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya michezo na uendelezaji wa vituo vya ufundi.

Infantino alitoa kauli hiyo jijini Rabat, Morocco, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Paul Makonda, kando ya mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).

Katika mazungumzo hayo, Waziri Makonda aliambatana na ujumbe wake kujadili namna ya kuboresha miundombinu ya soka nchini Tanzania. Infantino alieleza kufurahishwa kwake na ziara hiyo, akisisitiza umuhimu wa kutumia vyema mipango ya FIFA ili kufungua fursa za maisha kwa vijana kupitia mchezo wa soka.

Mambo makuu yaliyogusiwa katika mkutano huo ni pamoja na uimarishaji wa maendeleo ya msingi ambapo mkazo uliwekwa katika kukuza vipaji kuanzia ngazi za chini; Majadiliano yaligusia utekelezaji wa mradi wa uwanja wa FIFA nchini Tanzania na  uwekezaji wa serikali ambapo Waziri Makonda alielezea dhamira ya serikali kuwekeza kwenye miundombinu bora na programu za maendeleo ya vipaji, ikitambua soka kama chombo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Katika mazungumzo hayo Waziri Makonda aliongoza ujumbe uliowajumuisha viongozi waandamizi, akiwemo Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Gerson Msigwa; Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha; pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Morocco (mwenye makazi yake Paris, Ufaransa), Ali Jabir Mwadini.

No comments