RAIS SAMIA AMKARIBISHA PAPA LEO XIV KUTEMBELEA TANZANIA: AWEKA MSISITIZO KATIKA AMANI, UTU NA FALSAFA YA 4R
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasilisha ujumbe mzito wa kidiplomasia na kiroho kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, akisisitiza uthabiti wa Tanzania katika kudumisha amani, umoja, na utu.
Katika hatua inayolenga kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Vatican, Rais Samia amemwalika rasmi Baba Mtakatifu kuitembelea Tanzania wakati wowote atakaochagua, mwaliko unaolenga kuwapa tumaini jipya Watanzania na kuimarisha urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
Ujumbe huo wa Rais Samia uliwasilishwa jijini Vatican na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika maelezo yake, Balozi Kombo alibainisha kuwa Tanzania inathamini sana nafasi ya Papa Leo XIV kama sauti ya dunia katika kuhimiza amani,haki na kuthaminiana. Rais Samia ameweka wazi kuwa Serikali yake inazingatia mtazamo wa Baba Mtakatifu kwamba amani ya kweli si tu kutokuwepo kwa vurugu, bali ni uwepo wa haki na kujaliana kwa dhati kati ya wananchi.
Kwa mara nyingine, Rais Samia ametumia fursa hiyo kueleza dhamira yake ya dhati ya kuimarisha maridhiano nchini kupitia falsafa yake ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Kujenga Upya).
Balozi Kombo alieleza kuwa Serikali inasikitishwa na vifo na vurugu zilizotokea wakati wa kipindi cha uchaguzi, na kwa kufuata miongozo ya amani, Rais ameelekeza mamlaka husika kukabili hali hiyo kwa kuimarisha umoja na kuaminiana miongoni mwa Watanzania.
Aliongeza kuwa sauti ya Kanisa Katoliki imekuwa faraja kubwa nyakati za changamoto, na maneno ya Papa yanayohimiza majadiliano yana maana kubwa katika kudumisha utulivu wa kijamii.
Mbali na masuala ya amani na maridhiano, Serikali ya Tanzania imetambua na kupongeza mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za Kanisa Katoliki nchini. Balozi Kombo alibainisha kuwa mchango wa kanisa katika sekta za elimu, afya, na maendeleo ya jamii kwa ujumla ni nguzo muhimu inayosaidia juhudi za taifa katika kuwaletea wananchi maendeleo. Shukrani za pekee zilitolewa kwa Baba Mtakatifu kwa matumaini yanayoendelea kuletwa na kanisa hilo kwa mamilioni ya Watanzania.
Mwaliko huu kwa Papa Leo XIV unakuja wakati ambapo Tanzania inajipambanua kama kitovu cha amani na maridhiano katika ukanda wa Afrika Mashariki. Serikali inaamini kuwa ziara ya Baba Mtakatifu nchini Tanzania itakuwa ni fursa adhimu ya kuunganisha watu, kuhimiza haki, na kutoa mwongozo wa kimaadili utakaosaidia taifa kusonga mbele kwa umoja.
Balozi Kombo alisema kuwa Tanzania iko tayari kumpokea Kiongozi huyo wa Dunia ili kuendelea kuandika historia ya urafiki na mshikamano wa kimataifa.

Post a Comment