BONDIA FRANK SHAGEMBE ATWAA MKANDA WA AFRIKA (WBO)



Bondia Frank Shagembe kutoka mkoani Mbeya ameandika historia mpya katika medani ya ngumi nchini baada ya kutwaa mkanda wa Afrika wa WBO katika pambano la kusisimua la Knockout ya Mama msimu wa saba.

Shagembe alifikia mafanikio hayo kwa kumtandika mpinzani wake, Haruna Osumanu kutoka nchini Ghana, katika pambano lililofanyika juzi kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa kujiamini mara baada ya kutangazwa kuwa bingwa, Shagembe alieleza kuwa mpinzani wake alishindwa kuhimili kasi na uzito wa ngumi zake, hali iliyompelekea kuhitimisha pambano hilo mapema kabla ya raundi zote kumalizika.

Bondia huyo alisisitiza kuwa licha ya kuwa na mwili mdogo ukilinganisha na Osumanu, hakuwa na hofu yoyote kwani alijiandaa vyema chini ya benchi lake la ufundi na kupata usimamizi madhubuti kutoka kwa uongozi wake wa Mafia Boxing Promotion.

Shagembe alibainisha kuwa ushindi huo ni utimilifu wa malengo aliyojiwekea kwa asilimia 100 kabla ya kupanda ulingoni. Akizungumzia mustakabali wake, aliahidi kufanya makubwa zaidi huku akitamba kuwa kwa sasa hakuna bondia nchini anayeweza kumudu makonde yake, akidai kuwa mabondia wengi wamekuwa wakimkwepa ulingoni.

Aidha, bondia huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za kukuza sekta ya michezo nchini.

Usiku huo wa Knockout ya Mama ulikuwa na mfululizo wa matokeo ya kusisimua ambapo Yusufu Changarawe alimshinda Abdul Kisenga na kutwaa mkanda wa ubingwa wa Taifa wa TPBRC, huku Amiri Matumla naye akijitwalia mkanda wa TPBRC kwa kumpiga Sebastian Bau.

Katika mapambano mengine, Yohana Mchanja alimchakaza bondia kutoka Ufilipino, Renz Rosia, wakati Asemahle Wellem akijihakikishia ubingwa wa WBO Afrika baada ya kumshinda Emmanuel Martey.

No comments