MAAMUZI YA MWAMUZI TRAORÉ YAIBUA MJADALA: TAIFA STARS YAONDOKA KISHUJAA AFCON 2025



Safari ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, katika michuano ya AFCON 2025 nchini Morocco imefikia tamati kufuatia kichapo cha bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco, huku mchezo huo ukiacha sintofahamu na malalamiko mazito dhidi ya mwamuzi Boubou Traoré raia wa Mali.

Licha ya Morocco kuingia uwanjani wakiwa namba moja kwa ubora barani Afrika na kupewa nafasi kubwa ya kushinda, Stars walicheza kwa kiwango cha hali ya juu na kuwashikilia 'Simba wa Atlas' hadi dakika ya 64 pale Brahim Diaz alipopata bao pekee. 

Hata hivyo, mchezo huo ulitawaliwa na kashfa ya maamuzi baada ya mwamuzi Traoré kukataa kutoa penati ya wazi kwa Taifa Stars na kukataa hata kwenda kuitazama teknolojia ya usaidizi wa video (VAR) baada ya mchezaji wa Tanzania kuangushwa eneo la hatari.




Mashabiki wengi kupitia mitandao ya kijamii wameelezea kutoridhishwa kwao na mwamuzi huyo, wakidai kuwa amekuwa na upendeleo wa wazi kwa Morocco. 

Takwimu zinaonyesha kuwa Traoré amechezesha mechi nyingi za Morocco (8) kuliko timu nyingine yoyote ya taifa, huku akitoa penati tatu katika mechi hizo na Morocco ikishinda mechi zote za kimashindano chini yake. Mashabiki wamehoji kwa nini VAR ilishindwa kutumiwa kwa usawa kwa mataifa madogo katika soka kama Tanzania na Tunisia pindi yanapokutana na mataifa makubwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, amewapongeza vijana wa Stars kwa kupambana kiume. Msigwa amebainisha kuwa ingawa timu imetolewa, imetoka kishujaa huku ikijulikana kuwa lile lilikuwa ni "tuta" la wazi ambalo halikuhitaji hata VAR. Ameeleza kuwa Stars wameubonda mpira na kuwaonyesha waliowawazia wepesi kuwa Tanzania ina kitu cha tofauti na imecheza zaidi ya matarajio ya wengi.







Hisia za "wizi wa wazi" zimetawala miongoni mwa wachambuzi na mashabiki, wakiamini kuwa bila upendeleo kwa wenyeji, mchezo huo ungestahili kwenda kwenye hatua ya matuta. "Tumeachwa kinywa wazi, tumepambana na tumewashika, bila mbeleko tulistahili kusonga mbele," alisema mmoja wa mashabiki katika mjadala mtandaoni.

Pamoja na maumivu hayo, wadau wametoa rai kwa Taifa Stars kujiimarisha zaidi kuelekea mashindano yajayo kwani kiwango kilichoonyeshwa kimeacha heshima kubwa kwa soka la Tanzania barani Afrika. Wakati Morocco wakitinga robo fainali kwa mbinde, Tanzania imeondoka ikiwa imewacha doa katika ushindi wa wenyeji kutokana na utata wa mwamuzi Traoré.

No comments