Wasaga sumu waendelea kunyooka, watanzania wanajielewa

 





Kadiri siku zinavyosogea kuelekea kilele cha sikukuu za mwisho wa mwaka, imebainika wazi kuwa "vidonge" vya uzalendo na amani vimeanza kuwakolea wale wote wenye nia ovu ya kutaka kuivuruga nchi. Watanzania, kwa ukomavu wao wa hali ya juu, wameendelea kuonesha kuwa wanazijua janja za wachochezi wanaotaka kuiunguza nchi kwa maslahi yao binafsi na ya mabeberu.

Msimamo huu wa wananchi umekuwa pigo kubwa kwa makundi yanayojaribu kuhamasisha vurugu, kwani kama ambavyo watanzania hawakushiriki "ujinga" uliopangwa Desemba 9 , ndivyo ambavyo Desemba 25 itapita kwa amani na utulivu. Ujumbe umefika: Tanzania si uwanja wa majaribio ya fujo.

Katika kuunga mkono misingi ya nchi, kauli ya mzee maarufu na mshauri wa masuala ya uongozi, Mzee Joseph Butiku, imetoa mwelekeo chanya. Mzee Butiku amesisitiza kuwa Rais ameshachaguliwa na ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si Rais wa chama fulani pekee. Ni nguzo ya taifa na ni wajibu wa kila mzalendo kumlinda na kumheshimu kwa sababu anawakilisha utu na mamlaka ya nchi yetu.

Wale wanaopiga kelele wakitaka Rais "aondoke kesho" wanajidanganya. Watanzania hawajafanya kosa kumchagua kiongozi wao, na jitihada zozote za kutaka kumuondoa nje ya taratibu za kisheria na kikatiba hazitakubalika na hazitapata mwitikio wa umma. Tunazungumza juu ya Rais wetu kwa nia njema, kwa heshima, na kwa kuthamini kazi anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Licha ya kuwepo kwa maoni mseto kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu wanajaribu kumshambulia Mzee Butiku kwa kauli yake ya kishujaa, ukweli unabaki palepale: busara za wazee ndizo zinazolivusha taifa hili kwenye dhoruba. Mashambulizi dhidi ya wazee wanaosimamia ukweli ni ishara ya kukata tamaa kwa wale ambao mipango yao ya vurugu imefeli.

Wanaodai kuwa uchaguzi uliibiwa au Rais hatakiwi, ni kundi lilelile ambalo limekuwa likitumiwa kama vibaraka wa maslahi ya nje. Watanzania wa leo si "bendera fata upepo"; wanajua kutofautisha kati ya ukosoaji wenye tija na uhaini unaolenga kubomoa misingi ya amani tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa hili.

Tunapoelekea mwishoni mwa mwaka, kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake. Tuwapuuze wale wote wanaotumia lugha za kuudhi na uchochezi kwenye majukwaa ya kidijitali. Tunapaswa kukumbuka kuwa amani ikitoweka, hakuna atakayebaki salama—iwe mfuasi wa serikali au mpinzani.

Rais wetu ni alama ya umoja wetu. Hatukubali na hatutakubali kuyumbishwa na bahasha za mabeberu au ahadi za uongo kutoka kwa watu wasioitakia mema Tanzania. Desemba 25 itakuwa siku ya furaha, amani, na shukrani, na si siku ya kushiriki "miradi ya giza" ya watu wachache wenye njaa ya madaraka.


No comments