Vijana wahimizwa kunufaika na fursa: Vituo vya maendeleo ya vijana kuboreshwa




Vijana wanahimizwa kutambua na kufuatilia kwa karibu mipango ya serikali, hasa hatua za kuboresha vituo vya maendeleo ya vijana. Kwa kutumia vituo hivi, vijana wanaweza kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira na kuanzisha miradi yao wenyewe, na hivyo kutengeneza fursa za ajira kwao na kwa wengine.

Wito huo umetolewa wakati Serikali ya Tanzania imeainisha dhamira yake thabiti ya kuviboresha na kuvitumia kikamilifu vituo vya maendeleo ya vijana nchini ili viwe silaha muhimu ya kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii, na kielimu.

Desemba 15, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, akitembelea na kukagua utendaji kazi katika Kituo cha Vijana cha Sasanda kilichopo mkoani Songwe alibainisha kuwa kuna jumla ya Vituo vitatu vikuu vya Vijana nchini, vya Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro), na Marangu (Kilimanjaro). 

"Kituo hiki cha Sasanda kilitoa mafunzo kwa vijana tangu mwaka 1979 na mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2008. Kwa muda mrefu kimekuwa hakifanyi kazi. Ndiyo maana tumejipanga kuviboresha vituo hivi na kuhakikisha vinawasaidia vijana katika maeneo haya," alisema Mhe. Nanauka.

Alisisitiza viongozi wa mikoa ambako vituo hivi vipo kuviweka katika kipaumbele, akieleza kuwa ni maeneo yenye mazingira bora na fursa sahihi kwa vijana.

Waziri alikumbusha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa kipaumbele kikubwa kwa masuala ya Maendeleo ya Vijana, kiasi cha kuamua kuunda Wizara maalumu inayoshughulika na mambo yao. Hatua hii inaonyesha uwekezaji mkubwa wa Serikali katika mustakabali wa vijana.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Mapana, aliwakumbusha Watendaji wa Serikali kuendana na falsafa za Wizara, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kasi, kutembelea maeneo wanayopatikana vijana, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kufanikisha miradi ya vijana. 


No comments