Serengeti Boys Mabingwa wa CECAFA U-17, Wafuzu AFCON 2026




Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, 'Serengeti Boys', imenyakua ubingwa wa Mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya kuibamiza Uganda kwa ushindi wa mabao 3-2 katika fainali ya kusisimua iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Abebe Bikila nchini Ethiopia.

Ushindi huu umewafanya Serengeti Boys wawe timu pekee katika michuano hiyo kushinda mechi zote sita, wakifunga jumla ya mabao 30 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne pekee.

 Kisasi na Mfungaji Bora

Mabao ya Serengeti Boys katika fainali hiyo yalifungwa na Razack Juma aliyetikisa nyavu mara mbili, huku bao la tatu likiwekwa kimiani na Luqman Mbalasalu. Bao hilo limemwezesha Mbalasalu kufikisha mabao tisa (9) na kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa mashindano.

Ushindi huu ni kisasi kwa Serengeti Boys, kwani walipoteza dhidi ya Uganda kwa mabao 2-1 katika fainali ya mwaka 2024 iliyofanyika jijini Kampala.

Tiketi ya AFCON 2026

Licha ya ubingwa, habari njema zaidi kwa taifa ni kuwa Serengeti Boys imefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (AFCON U-17) mwaka 2026 kwa mara ya pili mfululizo. Serengeti Boys ilikata tiketi ya fainali baada ya kuifunga Kenya kwa mabao 3-1 katika nusu fainali.

Timu zilizofuzu kutoka Kanda ya CECAFA kwenda AFCON 2026 ni:Tanzania (Serengeti Boys) - Mabingwa;Uganda - Mshindi wa Pili na Ethiopia - Mshindi wa Tatu.

Ethiopia ilifuzu baada ya kuishinda Kenya kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu.

Michuano hiyo ilianza Novemba 15, mwaka huu, ikishirikisha timu 10 kutoka ukanda huu: Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Rwanda, Tanzania, Uganda, Sudan, Burundi, na Djibouti.

No comments