AFCON 2025 YAJA,AFRIKA MASHARIKI WATAKIWA KUITHAMINI



Kuelekea kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) nchini Morocco, viongozi wa masoko ya burudani wamehimiza nchi za Afrika Mashariki (E.A) kuacha kusherehekea ligi za mataifa mengine na kuelekeza nguvu zao katika kuthamini na kuwekeza katika mashindano haya makubwa ya soka barani Afrika.

Mashindano ya AFCON 2025 yanatarajiwa kuanza Januari 21 na kumalizika Februari 18 nchini Morocco, ambapo mechi zote 52 zitaoneshwa mubashara kupitia SuperSport.

Akizungumza Dar es Salaam, Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Multchoice Tanzania, Baraka Shelukindo, alisisitiza umuhimu wa kukuza utambulisho wa Kiafrika kupitia soka.

"Haya ni mashindano ya Afrika, tusherehekee Uafrika wetu," amesema Shelukindo.

AFCON: Zaidi ya Soka, Ni Utamaduni

Shelukindo alieleza kuwa Multchoice imeonesha dhamira ya dhati kwa kurusha mechi zote, akibainisha kuwa AFCON sio tu mashindano ya soka bali ni tukio linalobeba utamaduni, historia, na umoja wa Waafrika.

Kwa kutambua hilo, matangazo ya mashindano hayo yataenda kwa lugha mbalimbali, ikiwemo Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, na Kireno, ili kuwafikia kila shabiki barani.

Kwa Tanzania, ambayo ipo Kundi C, mechi zake zitapatikana kupitia kifurushi cha Bomba, ikiwa ni mkakati wa kuwafikia mashabiki wengi zaidi na kuwawezesha kuungana na Taifa Stars yao.

Daraja la Kibiashara na Maskauti wa Ulaya

Mbali na burudani na umoja, Shelukindo alisisitiza jinsi AFCON inavyotumika kama daraja muhimu la kiuchumi na kimasoko kwa wachezaji wa Afrika.

"AFCON inatumika kama jukwaa kwa wachezaji chipukizi na wale wanaong’ara barani kuonesha vipaji vyao kwa maskauti wa Ulaya wanaofuatilia kwa karibu michuano hii," alisema.

Alisisitiza kuwa kwa Tanzania, huu ni wakati wa kipekee kwa wachezaji wa Taifa Stars kujitangaza na kufungua milango ya kucheza Ligi kubwa Ulaya.

Hoja ya Kuthamini Mashindano Yetu

Hoja ya msingi iliyotolewa na Shelukindo inatutaka tuwekeze hisia na rasilimali zetu katika AFCON badala ya ligi za nje. Hii ndio sababu ya kimsingi ya kuthamini AFCON:

1.     Kukuza Utambulisho: Kusherehekea AFCON ni kusherehekea utambulisho wa Kiafrika na kujitambulisha kama taifa moja kupitia soka, kuachana na tabia ya kuiga kwingine.

2.    Fursa za Kiuchumi za Ndani: Kuthamini AFCON kunahamasisha matumizi ya ndani (kulipia vifurushi vya ndani, kutazama kwa pamoja), tofauti na ligi za nje ambazo faida zake huishia Ulaya.

3.    Kuongeza Thamani ya Wachezaji: Mashindano haya ndio njia pekee wachezaji wa Tanzania na Afrika kupandisha thamani yao na kupata mikataba mikubwa nje ya nchi.

4.    Ujenzi wa Umoja wa Familia: "Msimu wa AFCON ni wakati wa familia nzima kukutana, kuungana na kusherehekea utambulisho wa Kiafrika kupitia soka. Ndio maana tumesema, wanafamilia tuna kikao chimbo – ni DStv," alihitimisha Shelukindo, akihimiza matumizi ya vifurushi vya ndani.

 


No comments