Tanzania yaaga Kombe la Dunia la Wanawake la Futsal
TIMU ya taifa ya wanawake ya mchezo wa Futsal imemaliza safari yake katika michuano ya Kombe la Dunia baada ya kukubali kipigo cha mabao 9-0 kutoka kwa Japan kwenye Uwanja wa Philsports, Manila, leo Novemba 29.
Michuano hii inafanyika kwa mara ya kwanza, na Tanzania iliweka historia kwa kuwa miongoni mwa timu za kwanza kushiriki baada ya kupata tiketi yake kwenye michuano ya Afrika iliyofanyika nchini Morocco mwezi Mei mwaka huu.
Katika mechi hii ya mwisho kwa Kundi C, Tanzania ilihitaji ushindi ili kusonga mbele katika hatua ya robo fainali. Hata hivyo, kasi na uzoefu wa wachezaji wa Japan ulikuwa mkubwa. Japan iliongoza kwa mabao 3-0 hadi mapumziko kabla ya kufunga mabao mengine sita katika kipindi cha pili.
Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa ukubwa katika historia ya Japan kwa kutofungwa goli (clean-sheet). Rekodi yao ya awali ilikuwa ni kuwafunga Bahrain 13-0 mwaka 2018.
Ubora wa Ryo Egawa
Ryo Egawa alitofautiana na wachezaji wenzake kadhaa baada ya dakika 40 kwenye Uwanja wa PhilSports. Kiungo huyo (pivot) alisisitiza kwamba yeye si miongoni mwa wachezaji bora duniani. Wenzake hawakukubaliana naye kwani ushahidi ulikuwa ubora wa Egawa uliizamisha Tanzania, na sasa anaiwinda Brazil.
Zuhura Waziri, Mlinda Lango wa Tanzania akizungumzia mechi hiyo alisema:“Tulijitahidi kutaka kufika robo fainali, lakini Japan ni timu nzuri sana. Sisi ni wageni kwenye mchezo huu. Imekuwa ni uzoefu wa ajabu. Kucheza Kombe la Dunia ni ndoto.”
Naye Naomi Matsumoto, Winga wa Japan alisema:“Nadhani tulicheza vizuri sana. Tunafurahi sana kushinda na tunafurahia mno kucheza dhidi ya Brazil. Walitufunga mwaka jana, kwa hivyo sasa ni zamu yetu kulipa kisasi na kuwafunga.”
Magoli ya Japan yalifungwa na Ryo Egawa,Naomi Matsumoto,Mizuki Nakamura,Kaho Ito,Yuka Iwasaki,Kyoka Takahashi na Anna Amishiro.Mchezaji Bora wa Mechi alikuwa Ryo Egawa
Kwa ushindi huo, Japan inaungana na Ureno kufuzu robo fainali kutoka Kundi C. Tanzania inamaliza nafasi ya tatu kwa pointi tatu, huku New Zealand ikimaliza bila pointi yoyote baada ya kufungwa 10-0 na Ureno katika mchezo wake wa mwisho uliofanyika leo.
Kocha Reid: Wachezaji Wanajivunia Uzoefu
Akizungumza baada ya mechi, Kocha Mkuu wa Tanzania, Curtis Reid, alieleza kufurahishwa kwake na maendeleo ya wachezaji wake na akawasihi wajivunie ushiriki wao.
“Sio kila mtu anaweza kucheza Kombe la Dunia, lakini wao (wachezaji) wameweza… ninachofurahi zaidi ni kwamba wanaimarika, hata kama tunapoteza mechi lakini naona mabadiliko kwao,” alisema Reid.
Alishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sapoti kubwa waliyoitoa kwa timu hiyo na akaliomba liendelee kuweka mikakati thabiti kwa maendeleo ya mchezo huo.
Ratiba ya Robo Fainali
Mechi za robo fainali zitaanza kuchezwa Desemba Mosi:
Argentina vs Colombia
Hispania vs Morocco
Brazil vs Japan
Timu nyingine zitakazokutana katika hatua hiyo zinatarajiwa kujulikana baadaye leo baada ya kumalizika kwa mechi zote za hatua ya makundi.

Post a Comment