Miss World Tanzania 2025 Yazinduliwa Rasmi Dar es Salaam





361 Degrees , inayoongozwa na mbunifu maarufu wa mitindo yenye kuakisi  utamaduni, Mustafa Hassanali, imezindua rasmi mashindano ya Miss World Tanzania 2025.

Jukwaa hilo limejikita katika kuwajenga na kuwawezesha wanawake vijana wa Kitanzania kuliwakilisha taifa kwa heshima, urembo, akili, na dhamira. 

Uzinduzi huo ulifanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Bwana Edward  Buganga.

Uzinduzi huu unaashiria mwanzo wa kipindi kipya chenye mwelekeo mpya na wa kisasa kwa shindano hili lenye hadhi kubwa.Miss World Tanzania inalenga kuwatambua na kuwalea wanawake vijana wenye uwezo wa kipekee wanaoonesha umahiri,uongozi na falsafa ya kimataifa ya Miss World ya Uzuri Wenye Kusudi (Beauty with a Purpose).

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mustafa Hassanali, ambaye anahudumu kama Mkurugenzi wa Kitaifa wa Miss World Tanzania, alisisitiza dhamira ya mashindano hayo: "Miss World Tanzania si shindano tu; ni fursa ya kubadilisha maisha ya vijana wa kike nchini. Dhamira yetu ni kutoa jukwaa linalokuza sauti zao kuimarisha jamii zao na kuwaandaa kuiwakilisha Tanzania kwa fahari na ubora katika jukwaa la kimataifa la Miss World"

Hassanali alisisitiza kuwa vigezo vya uteuzi vitaweka kipaumbele kwa washiriki wanaoonesha uwezo mkubwa wa uongozi, kujitolea katika huduma za jamii, na malengo ya kielimu, na si kuangalia tu mwonekano wa nje.

Naye Bwana Buganga, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, alitoa baraka kamili za Baraza hilokwa shindano hilo, akibainisha umuhimu wa kimkakati wa mashindano hayo.

"Tunaipongeza 361 Degrees Africa kwa kuchukua jukumu hili muhimu," alisema Bwana Buganga. "Ushirikiano wa BASATA na Miss World Tanzania ni muhimu ili kuhakikisha mashindano yanaambatana na viwango vya utamaduni wa kitaifa na kutoa mazingira yaliyopangika, yenye kuunga mkono, na ya kitaalamu kwa wanawake hawa wanaotamani kushiriki. Mashindano haya ni nyenzo yenye nguvu ya uwezeshaji wa vijana na fursa ya kuinua hadhi ya sanaa na burudani ya Tanzania kimataifa."

Waandaaji walitoa wito kwa wazazi  kukubali vijana wao kushiriki katika shindano hili kwani linatengeneza fursa. Aidha kampuni au vikundi vinavyotaka kushiriki katika mkutafuta washiriki wa ngazi ya kitaifa kutoka mikoani kutembelea tovuti na mitandao ya kijamii ya Miss World Tanzania kwa maelezo zaidi.

Dira ya 361 Degrees  kwa Miss World Tanzania iko wazi ni kuwa jukwaa endelevu ambalo litaendelea kuwajenga na kuwawezesha wanawake vijana wa Kitanzania, kuwaruhusu kuliwakilisha taifa kwa utofauti, heshima, akili, na malengo thabiti.

Imeelezwa katika mkutano huo na waandishi wa habari utafutaji wa Miss World Tanzania 2025 unaanza mara moja. Wanawake vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 25, na wenye kiwango cha chini cha elimu, pamoja na kujitolea katika kazi za jamii, wanahimizwa kuomba. Fomu za maombi na mahitaji ya kina ya kustahili yanapatikana mtandaoni kupitia majukwaa rasmi ya kidijitali ya Miss World Tanzania.

Mchakato wa uteuzi utafanyika katika wiki zijazo, ukihusisha usaili wa kitaifa na mafunzo ya kina kwa wagombea waliochaguliwa. Safari hii itahitimishwa katika Fainali Kuu inayotarajiwa  kufanyika Dar es Salaam.

Mshindi hatapokea tu zawadi muhimu za kitaifa bali pia atapewa haki na leseni ya kipekee ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kifahari ya kimataifa ya Miss World 2026.

No comments