CAF YAMPA TUZO RAIS SAMIA KUTAMBUA MCHANGO WAKE MAENDELEO YA KANDANDA
RAIS Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ikiwa ni kutambua mchango wake katika maendeleo ya kandanda.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Mji wa Rabat nchini Morocco jana.
Pamoja na Msigwa, hafla hiyo ya utoaji wa tuzo ilihudhuriwa na Rais wa TFF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Wallace Karia na Mwenyekiti wa klabu Afrika na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said.
Tuzo hiyo inatolewa kwa Rais Samia kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha uongozi wake ya ujenzi wa miundombinu ya michezo vikiwemo viwanja vikubwa, kuwa wenyeji wa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani (CHAN 2024) na maandalizi ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) pamoja mafanikio makubwa ya Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
Mafanikio hayo ni pamoja na kupanda kwa ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo sasa ni ya tano kwa ubora Afrika, kuboresha soka la wanawake na kukuza soka kwa vijana.
Pia mwaka huu Tanzania ni miongoni mwa mataifa matatu ambayo imeingiza timu nne kwenye mashindano ya Afrika pamoja na Misri na Morocco. Timu hizo ni Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa na Azam FC na Singida Black Stars Kombe la Shirikisho.
Mwaka jana pia timu za Taifa saba zilifuzu mashindano ya Afrika.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo Msemaji mkuu wa serikali alimshukuru Rais Samia kwa kupaisha jina la Tanzania katika michezo hasa ulimwengu wa soka .
Naye Rais wa TFF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Wallace Karia alimpongeza Rais samia kwa tuzo hiyo akisema kwamba anaistahili kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika michezo.
Alisema yeye binafsi na wapenzi wa soka wamefurahi mno kwa tuzo hiyo huku wakijua kwamba kuna mipango mingi ya serikali ya awamu ya sita inaandaliwa kwa ajili ya kulipaisha Taifa la Tanzania katika michezo.
Mwisho


Post a Comment