Tuchel akerwa na mashabiki England

 


Kocha Mkuu wa England, Thomas Tuchel, ameelezea masikitiko yake makubwa kwa kile alichokiona kama hali ya ajabu kwenye Uwanja wa Wembley hivi karibuni, ambapo timu yake iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Wales, lakini akasema alikuwa anasikia sauti za mashabiki wa wageni zaidi ya wenyeji.

Tuchel alisema mashabiki wa England walikuwa kimya kiasi kwamba walisikika mashabiki 7,000 waliosafiri kwenda London kuishangilia Wales. Hali hii ilimkera kocha huyo wa England, hasa kutokana na ukweli kwamba timu ilipata ushindi huo wa mabao 3-0 ndani ya dakika 20 za kwanza.

Akizungumza na ITV Sport baada ya mchezo huo wa kwanza uwanjani Wembley tangu Machi, Tuchel alionyesha kuchukizwa na utulivu uliojitokeza jukwaani:

“Tungeweza kupata mabao 5-0 mpaka kipindi cha kwanza. Hatukuweza kufunga bao la nne na la tano. Uwanja ulikuwa kimya. Hatukupata kuungwa mkono na mashabiki wetu jukwaani. Tulifanya kila linalowezekana kushinda mchezo huu,” alilalama Tuchel.

Kocha huyo Muingereza alisisitiza kuwa kiwango cha timu uwanjani kilihutaji shukrani na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini walishindwa kufanya hivyo.

“Tulitarajia zaidi kutoka kwa mashabiki. Hakuna zaidi unachoweza kufanya ndani ya dakika 20 zaidi ya kupata mabao haya? Hatukuweza kuwaachia wakimbie. Kama uliweza kusikia sauti za mashabiki wa Wales zaidi, inasikitisha kwa sababu timu hii ilistahili kuungwa mkono leo hii,” aliongeza Tuchel.

Alisifu Sapoti ya Serbia, Alikemea Ukimya wa Wembley

Hata hivyo, Tuchel hakusita kuonesha kufurahishwa kwake na namna mashabiki wa England walivyoishangilia timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Serbia ugenini, akitumia mfano huo kuongeza uzito wa malalamiko yake.

“Nimesema walishangilia vizuri kwenye mchezo dhidi ya Serbia ugenini. Nilisema hilo na nilimaanisha. Nawapenda mashabiki wa soka wa England na namna wanavyotuunga mkono. Lakini leo hawajashangilia kwa nguvu kwa kadiri ya kiwango tulichokionesha uwanjani,” alisema Tuchel kwa msisitizo.

Tuchel alimalizia kwa kutoa wito kwa mashabiki kubadilisha mtindo huo na kuunga mkono timu kwa nguvu zote, akisema: “Tunatakiwa kuishangilia timu itakapokwenda kucheza na Latvia kama walivyofanya kule Serbia. Lakini leo tulikuwa tunaongoza kwa mabao 3-0 mpaka dakika ya 20 lakini walikuwa kimya. Wangeweza kutusaidia kwenye nyakati fulani kama wangeshangilia kipindi cha pili.”

Malalamiko haya ya Tuchel yanaleta mjadala mkubwa nchini England kuhusu ni kwa jinsi gani mashabiki wanapaswa kuunga mkono timu yao, hata kama uwanja ulikuwa na idadi ndogo ya mashabiki waliohudhuria.

No comments