INEC Yafuta Kata 10, Yatengua Wagombea 7 wa Chama cha Mapinduzi



Na Mwandishi Wetu

 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya Tanzania imefanya marekebisho makubwa katika orodha ya maeneo ya uchaguzi kufuatia uamuzi wa Serikali kufuta kata kumi (10) katika mikoa ya Katavi na Tabora. Uamuzi huo umesababisha kufutwa kwa kata kumi kutoka katika maeneo ya uchaguzi wa madiwani na kutenguliwa kwa uteuzi wa wagombea udiwani saba (7) waliokuwa wameteuliwa katika kata hizo.

Marekebisho haya yametangazwa leo tarehe 12 Oktoba, 2025, na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs C.M. Mwambegele.


Asili ya Uamuzi

Ufufutaji wa kata hizo unatokana na matangazo mawili ya Serikali:

Tangazo la Serikali Na. 596 la tarehe 03 Oktoba, 2025, lililotangaza maeneo ya Ulyankulu (Kaliua, Tabora), Katumba na Mishamo (Tanganyika, Katavi) kuwa maeneo tengefu kwa ajili ya makazi ya wakimbizi.

Tangazo la Serikali Na. 600 la tarehe 03 Oktoba, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alitoa Amri ya Marekebisho ya Amri ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala, ikizifuta kata kumi (10).

Kata zilizofutwa ni pamoja na Litapunga, Kanoge, Katumba pamoja na vijiji viwili (Ikolongo na Ndurumo) vya Kata ya Mtapenda, zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Katavi. Kata nyingine zilizofutwa ni Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga (Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Katavi) na Milambo, Igombemkulu, Kanindo (Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Tabora).

Kulingana na Sheria ya Serikali za Mitaa (Sura ya 287), na masharti ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume ililazimika kufanya marekebisho kwani kufutwa kwa kata huondoa eneo la uchaguzi. Uamuzi huo ulifanyika katika kikao cha Tume kilichofanyika tarehe 06 Oktoba, 2025.


Wagombea Waliotenguliwa Uteuzi

Tume imetengua uteuzi wa wagombea udiwani saba (7) waliokuwa wameteuliwa katika kata saba zilizofutwa. Wagombea wote waliotenguliwa wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kata tatu za Milambo, Igombemkulu na Kanindo za Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua hazikuwa zimefanya uteuzi wa wagombea Udiwani.

Orodha ya wagombea waliotenguliwa ni kama ifuatavyo:

Salehe Mrisho Msompola (Kanoge)

Elius Wilson Elia (Katumba)

Mohamed Ally Asenga (Litapunga)

Nicas Athanas Nibengo (Bulamata)

Sadick Augostino Mathew (Ilangu)

Rehani Simba Sokota (Ipwaga)

Juma Mohamed Kansimba (Mishamo)


Kufutwa na Kuhamishwa kwa Vituo vya Kupigia Kura

Kutokana na mabadiliko hayo, Tume imevifuta vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa katika kata zilizofutwa. Hata hivyo, ili kuwawezesha wapiga kura kutumia haki yao, Tume imeanzisha vituo 292 vipya katika maeneo jirani.

Jumla ya wapiga kura 106,288 waliokuwa kwenye vituo vilivyofutwa wamehamishiwa kwenye vituo hivyo vipya 292.

Wapiga kura hao wamehamishiwa katika kata zifuatazo:


Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Katavi: Kata za Mtapenda, Uruwira, Nsimbo, na Ugala.

Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Tabora: Kata za Sasu, Ilege, Uyowa, Makingi, na Silambo.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Katavi: Kata ya Tongwe.


Wito kwa Wananchi


Tume imetoa wito kwa wananchi kuzingatia marekebisho haya ya maeneo ya uchaguzi ili waweze kushiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.

"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA"


No comments