KURA YA KIJANA NI ZAIDI YA KUTIKI
Na Mwandishi Wetu
Kizazi kipya
kinachoingia kwenye sanduku la kura kina nguvu isiyo na kifani ya kuunda
mustakabali wa Tanzania.
Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 29 si tu zoezi la kisiasa la mara moja; ni mchakato muhimu wa
kidemokrasia unaokupa wewe, kama kijana, jukumu la kubrandi (kuhakikisha
utambulisho) na kuielekeza nchi katika njia unayoitaka.
Wakati maneno ya
"Kura ni haki yako, na amani ni wajibu wako" yakisisitizwa, umuhimu wako
unakwenda mbali zaidi ya kupiga kura tu—unahusu kuona mchakato huu kama chombo
cha kujiletea mabadiliko.
Umuhimu wa Kura
Yako kwa Kizazi Kipya
Kama injini ya
ukuaji wa taifa, kizazi kipya kinapaswa kuona umuhimu wa kushiriki kikamilifu
katika uchaguzi kutokana na sababu hizi za msingi:
Kuamua Ajira na
Uchumi wa Kesho
“ Sisi vijana ndio
wenye changamoto nyingi zaidi. Mimi bado nasoma lakini naona kwamba ajira ni
changamoto. Sasa ni lazima tujue kwa muda mfupi au mrefu nani atasaidia
kuzalisha ajira au hata kutambua kwa hakika kwamba mitaala hii inatusaidia.
Kupiga kura kutasaidia kuingiza watu sahihi kwa ajili yetu” anasema Raphael
Mashilingi.
Vijana ndio kundi
kubwa linalokabiliwa na changamoto ya ajira. Kura yako haichagui tu Rais;
inachagua sera za kiuchumi zitakazojenga viwanda, kuwekeza katika teknolojia
(TEHAMA), na kuongeza fursa za mikopo kwa vijana.
“Nawasihi vijaa
wenzangu twende kumchagua kiongozi ambaye atatoa majibu ya vitendo kuhusu jinsi
atakavyopunguza ukosefu wa ajira na kuwafanya vijana kuwa waajiri, si
waajiriwa” anasema Mashilingi.
Maelezo yake
yanatokana na ukweli kuwa mchakato wa kidemokrasia unakupatia fursa ya kuchagua
mipango inayokidhi mahitaji ya kizazi chako.
Kuunda Utambulisho
Mpya (Branding the Nation)
Kizazi kipya
ndicho cha kwanza kukua kikamilifu katika enzi ya kidigitali. Kushiriki kwako
katika uchaguzi, kwa amani na utulivu, kunatoa picha chanya ya Tanzania kwa
ulimwengu. Unachagua kuifanya nchi yako ibrandiwe kama taifa la Kidemokrasia,
lenye utulivu, na linaloheshimu utawala wa sheria. Utulivu huu ndio huvutia
wawekezaji, na hatimaye, huleta ajira unazozihitaji.
Wajibu Wako: Zaidi
ya 'Kutiki'
Uchaguzi wa Oktoba
29 unakuhitaji uwe zaidi ya mpiga kura anayekwenda kutiki (kuweka alama).
Unahitaji kuwa balozi wa mchakato wa kidemokrasia.
• Piga Kura na Linda Amani: Amani Yetu
Kwanza haipaswi kuwa kaulimbiu tupu. Kushiriki kwako kunapaswa kuambatana na
kukataa vurugu na matusi ya mitandaoni. Hakuna siasa inayofaa kusababisha
uvunjifu wa amani.
• Chagua Sera, Sio Mihemko: Jikite katika
kuchambua sera na kujua mgombea anasema nini kuhusu afya, elimu, na ajira.
Epuka mihemko, badilisha hisia kuwa uamuzi wenye tija.
Kizazi kipya
ndicho kinaletwa mezani kwa sasa na maamuzi ya nchi hii. Kwa hiyo, toka na
ukapige kura Oktoba 29. Nenda kwa amani, na uonyeshe kuwa kura yako inajenga
Tanzania unayoitaka.

Post a Comment