CRISTIANO RONALDO AWEKA REKODI YA KUWA BILIONEA WA KWANZA KISOKA DUNIANI!

 



Hadithi ya soka imeandikwa upya! Cristiano Ronaldo, gwiji wa Ureno na mshambuliaji wa klabu ya Al-Nassr ya Saudi Pro League, sasa amekuwa mwanasoka wa kwanza kabisa katika historia kufikia hadhi ya bilionea duniani, kwa mujibu wa kampuni ya habari na kifedha ya Bloomberg.

Faharasa ya Mabilionea ya Bloomberg, ambayo hufuatilia utajiri wa watu matajiri zaidi duniani kulingana na mali zao halisi, imepima utajiri wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 kwa mara ya kwanza na kuthibitisha kwamba sasa ana utajiri halisi wa Dola bilioni 1.4 (takriban Shilingi trilioni 3.5 za Tanzania).

Hesabu hii inazingatia mapato yake yote ya kazi, uwekezaji, na mikataba ya matangazo.

Taarifa hiyo inaonesha kuwa Ronaldo alijikusanyia zaidi ya Dola milioni 550 (takriban Shilingi bilioni 1.37) kupitia mshahara pekee kati ya mwaka 2002 na 2023. Zaidi ya hayo, inabainisha mikataba yake mikubwa ya udhamini, ikiwemo mkataba wa miaka kumi na kampuni ya Nike wenye thamani ya takriban Dola Milioni 18 (Shilingi Bilioni 45) kwa mwaka.

Mambo yalimwendea vyema zaidi Ronaldo alipojiunga na Al-Nassr mwaka 2022, ambapo inaripotiwa kuwa alipata mshahara mkubwa zaidi katika historia ya soka duniani, ukiwa na thamani ya takriban Pauni milioni 177 kwa mwaka.

Hivi karibuni, alitia saini mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya zaidi ya Dola milioni 400 (takriban Shilingi trilioni 1), ambao unamfanya abaki klabuni hapo hata baada ya kutimiza umri wa miaka 42.

Messi Naye Yuko Karibu

Licha ya Ronaldo kupiga hatua hii kubwa, mpinzani wake wa jadi, Lionel Messi, mshambuliaji wa Argentina na Inter Miami, naye yuko kwenye ramani ya matajiri.

Bloomberg inasema Messi, mwenye umri wa miaka 38, amepata zaidi ya Dola milioni 600 (takriban Shilingi bilioni 1.5) katika mshahara kabla ya kodi katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.

Hata hivyo, mapato yake ya sasa ya Inter Miami, ambapo anapata takriban Dola milioni 20 kwa mwaka, ni asilimia 10 tu ya kile ambacho Ronaldo anakipata Al-Nassr katika kipindi hicho hicho.

Ikumbukwe kwamba Messi, atakapostaafu, anatarajiwa kupata hisa katika klabu yake ya Inter Miami, hatua itakayomweka kwenye orodha ya matajiri wakubwa wa michezo kwa miaka mingi ijayo.

No comments