TAFF YAKABIDHI ZAWADI KWA TIMU BORA ZA SOKA KWA WATU WENYE ULEMAVU



Dar es salaam - Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu (TAFF) limekabidhi zawadi kwa timu zilizofanya vizuri katika mashindano ya soka kwa watu wenye ulemavu yaliyofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliyodumu kwa siku tatu yalishirikisha timu nane kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo Ubungo FC iliibuka bingwa na kujinyakulia zawadi ya Shilingi milioni moja. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Sauti Parasports ambayo ilizawadiwa Shilingi 500,000, huku Arusha Warriors ikishika nafasi ya tatu na kupokea Shilingi 250,000.

Mbali na zawadi hizo, kila timu iliyoshiriki mashindano hayo ilipatiwa Shilingi 400,000 kwa ajili ya kusaidia mahitaji mbalimbali, pamoja na kugharamiwa usafiri, malazi na chakula.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi, nahodha wa Ubungo FC, Frank Ngairo pamoja na Ashraf Alombile wa Sauti Parasports walishukuru kwa kupatiwa zawadi zao kwa wakati, huku wakitoa pongezi kwa Azam TV kwa udhamini wao na kwa kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa TAFF, Rahel Pallangyo alizipongeza klabu zote zilizoshiriki na kuwashukuru Azam TV kwa kudhamini mashindano hayo. Alitoa wito kwa wadau na wadhamini wengine kujitokeza zaidi, akisisitiza kuwa watu wenye ulemavu nao wana haki ya kushiriki na kunufaika na michezo kama watu wengine.

Timu zilizoshiriki mashindano hayo ni Ubungo FC, Sauti Parasports na Pugu Para kutoka Dar es Salaam; Magharibi A kutoka Unguja; Arusha Warriors na Black Eagle kutoka Arusha; pamoja na timu kutoka Songwe na Wilaya ya Mjini ya Zanzibar.

No comments