IVO MAPUNDA ATEULIWA KOCHA MKUU WA TEMBO WARRIORS




Na Mwandishi Wetu - Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu (TAFF) limemtangaza rasmi Ivo Mapunda kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu, Tembo Warriors.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TAFF, Shaban Msangi, ambaye amesema Mapunda atahudumu katika nafasi hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku mafanikio yake yakifuatiliwa kwa karibu.

Kwa mujibu wa Msangi, uteuzi wa Mapunda unakuja wakati Tembo Warriors wakijiandaa kushiriki michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAAF) inayotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu huko Bujumbura, Burundi. Msangi amesema kuwa Jumatatu ijayo, Mapunda atakutana na viongozi wa TAFF kupanga tarehe rasmi ya kutangaza kikosi cha timu ya Taifa.

Mapunda, ambaye ni mchezaji wa zamani wa klabu za Simba, Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, aliwahi pia kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Tembo Warriors mwaka 2022 kama kocha wa makipa katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Uturuki.

Uteuzi huu unaleta matumaini mapya kwa Tembo Warriors huku wakijiandaa kwa kampeni ya kutetea heshima ya taifa katika michuano ya kimataifa.

No comments