MVUA
kubwa iliyonyesha jana jioni ikiambatana
na upepo mkali ilisababisha kukatika kwa umeme kwenye uwanja wa Taifa Dar es
Salaam na kufanya mechi ya Simba na Al Masry ya Misri kusimama kwa takriban
dakika 30.
Mechi hiyo ya kombe la Shirikisho Afrika ilisimama zikiwa zimesalia
dakika 12 kumalizika, huku timu hizo zikiwa sare ya kufungana mabao 2-2. Hata
hivyo baada ya mvua kukatika na umeme kurudi uwanjani hapo, waamuzi waliamuru
mechi iendelee kwa dakika ilizosimama ambapo ilimalizika kwa matokeo hayohayo ya
2-2.
Hii si mara ya kwanza kwa Simba yenye historia ya kutofungwa na timu za
waarabu nyumbani kukutana na dhahama ya mvua na mechi kuahirishwa ama kusimama.
Mwaka 2001 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, ilikutana na dhahama hiyo
kwenye uwanja wa Uhuru (Zamani taifa) ambapo mechi yake dhidi ya Ismaili ya
Misri iliahirishwa kutokana na mvua kubwa ambapo mpaka mapumziko Simba ilikuwa
mbele kwa mabao 2-0
yaliyofungwa na Joseph Kaniki na Shekhan Rashid.
Kwa mujibu wa kanuni za
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakati huo, mechi ikiahirishwa inarudiwa yote
baada ya saa 48, hivyo mechi hiyo ilirudiwa baada ya siku mbili ambapo Simba
ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Kaniki, lakini iliondolewa kwenye michuano
maana katika mechi ya kwanza iliyochezwa Misri Ismaili ilishinda mabao 2-0.
Kwa
matokeo hayo ya jana, Simba inahitaji kupata ushindi wa aina yoyote ugenini
wiki ijayo, au itoke sare ya zaidi ya mabao mawili. Simba ilikuwa ya kwanza
kupata bao la kuongoza katika dakika ya nane likifungwa na nahodha wake John Bocco
kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi baada ya mchezaji wa Al Masry
Mohammed Koffi kunawa mpira eneo la hatari.
Bao hilo lilidumu kwa dakika mbili
tu kabla ya Masry kusawazisha kupitia
kwa Ahmed Gomaa akiunganisha krosi ya Mohamed Ahmed. Al Masry walipata bao la
pili katika dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi baada ya
James Kotei kunawa mpira kwenye eneo la hatari. Penalti hiyo ilikwamishwa
wavuni na Ahmed Abdalraof.
Katika
kipindi chote cha kwanza Simba ilionekana kuzidiwa na wageni walifanya
mashambulizi langoni kwao mara kwa mara. Simba, ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma
kwa mabao 2-1 jambo lililofanya benchi lake la ufundi kufanya mabadiliko dakika
chache baada ya kuanza
kwa kipindi
cha pili ambapo alitoka Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.
Awali, kabla ya kutoka Bocco, benchi la ufundi liliamua atoke Shizza Kichuya,
lakini mchezaji huyo pamoja na wenzie waliokuwa uwanjani waligoma na kushauri
asitoke ndipo ilipoamuliwa
atoke Bocco.
Mabadiliko hayo yalirudisha uhai kwa Simba ambapo sasa walipeleka mashambulizi
mfululizo langoni mwa Al Masry ambapo Kichuya na Okwi walikosa mabao kwa
nyakati tofauti kwa kupiga mipira ya juu wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga.
Emmanuel
Okwi aliisawazishia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na
mwamuzi baada ya Koffi wa Masry kushika mpira eneo la hatari. Dakika chache
baada ya bao hilo ndipo mvua kubwa iliponyesha na kusababisha umeme kukatika
hali iliyozua mtafaruku.
No comments:
Post a Comment