SIMBA, leo imeendeleza msemo wake wa 4G mpaka kwenye michuano ya kimataifa baada ya
kuifunga Gendarmerie mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa
Dar es Salaam.
Katika mechi
hiyo ya michuano ya kombe la Shgirikisho Afrika, Simba ilifunga mabao matatu
katika kipindi cha kwanza huku bao la nne ikilifunga dakika za mwisho za
kipindi cha pili.
Wawakilishi
hao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho walianza kuhesabu mabao dakika ya
kwanza ya mchezo huo baada ya Said Ndemla kufunga kwa mpira wa adhabu
uliokwenda moja kwa moja kutikisa nyavu.
Nahodha wa
Simba, John Bocco alifunga mabao mawili katika mechi hiyo, dakika ya 32
alilolifunga baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Gendarmerie na dakika
ya 45 alipofunga bao la kichwa akiunganisha krosi ya Emmanuel Okwi.
Simba
ilitawala katika kila idara kwenye kipindi cha kwanza, lakini hali ilibadilika
kwenye kipindi cha pili baada ya wapinzani wao kuonekana kujizatiti zaidi.
Kujizatiti
huko kwa Gendarmerie kuliwafanya Simba kupata tabu kuongeza mabao, hasa Okwi
aliyeonekana kutatizika anapopiga mipira ya adhabu.
Pengine
baada ya kujiuliza na kujirekebisha, dakika ya 90, Okwi aliandika bao la nne
kwa Simba kwa mpira wa adhabu ulioanzishwa na Erasto Nyoni kabla ya ‘Mhenga’
huyo kuuwahi na kuujaza wavuni.
Shujaa
mwingine katika mechi ya jana alikuwa kipa wa Simba, Aishi Manula aliyeoangua
penalti katika dakika ya 50.
Penalti hiyo
iliyopigwa na Abdorahim Mohammed ilitolewa na mwamuzi baada ya James Kotei wa
Simba kumchezea rafu Ahamed Aden wa Gendarmerie.
Matokeo hayo
yanaiweka Simba nafasi nzuri ya kusonga mbele kwani sasa wapinzani wake
watalazimika kushinda 5-0 katika mechi ya marudiano ili wasonge mbele.
Akizungumza
baada ya mechi hiyo, nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamefurahia matokeo
hayo na sasa wanaiandaa na mechi za Ligi Kuu kwani lengo lao ni kufanya vizuri.
Nahodha wa
Gendarmerie alisema moja ya sababu za wao kupoteza mechi hiyo ni hali ya hewa
ya joto kali.
“Simba ni
timu kubwa, tumefurahi tumepata uzoefu zaidi nasi tutajipanga kwa mechi ijayo,
huwezi jua kwenye soka lolote linaweza kutokea,” alisema.
No comments:
Post a Comment