EMMANUEL
Okwi aneipatia Simba pointi muhimu baada ya kuifungia bao katika ushindi
wa 1-0 dhidi ya Azam kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Taifa.
Ushindi huo
unaifanya Simba izidi kujikita kileleni kwa kujikusanyia pointi 41 juu ya Azam
na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 34 na Azam yenye pointi 33.
Iliichukua
Simba dakika 37 kuandika bao pekee katika mechi hiyo ambayo vinara hao wa ligi
walitawala zaidi kipindi cha kwanza.
Okwi
alifunga bao hilo baada ya kuunganisha krosi safi ya Asante Kwasi kabla ya
kuujaza mpira wavuni.
Kabla ya
kufunga bao hilo, Okwi ‘Mhenga’ alipata nafasi kadhaa za kufunga katika dakika
ya 5, 24 na 28 ambapo zote ama zilidakwa na kipa wa Azam, Razak Abalora au
zilitoka nje.
Azam
ilionekana kubadilika katika kipindi cha pili ambapo benchi lake la ufundi
lilianza kwa kufanya mabadiliko kwa kumtoa Mbaraka Yusuf na kumuingiza Shaaban
Iddi.
Mabadiliko
hayo yaliifanya timu hiyo kubadilika kwani sasa mashambulizi yalifika langoni
mwa Simba na dakika ya 49 Yahaya Zaud alipata nafasi lakini alipiga mpira
pembeni.
Aidha katika
mechi hiyo kulikuwa na ubabe wa hapa na pale ikiwa ni pamoja na mfungaji wa bao
la Simba Okwi kufanyiwa madhambi ya mara kwa mara na mabeki wa Azam.
Pengine hiyo
ndiyo sababu ya benchi la ufundi la Simba kumtoa nyota huyo wa Uganda katika
dakika ya 84 na nafasi yake kuchukuliwa na Nicholas Gyan.
Katika mechi
nyingine za ligi zilizochezwa jana, Mwadui imeutumia vema uwanja wake wa
nyumbani kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1 huku Mbao ikishindwa kufanya hivyo
kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1.
Simba: Aishi
Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Yussuph Mlipili, Asante Kwasi, Jonas
Mkude, Shiza Kichuya, Said Ndemla/Muzamil Yassin dk59, John Bocco, Emmanuel
Okwi/Nicholaus Gyan dk84, James Kotei.
Azam FC:
Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris,
Stephan Kingue, Iddi Kipagwile/Salum Abubakar dk55, Frank Domayo, Mbaraka
Yussuph, Yahya Zayed/Bernard Arthur dk71, Enock Atta-Agyei.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment