Kamati ya Nidhamu iliyokutana Jumamosi Februari 10, 2018
pamoja na mambo mengine pia ilipitia shauri la mchezaji wa Kagera Sugar Juma
Nyoso lililofikishwa kwenye kamati akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu kwenye
mechi namba 112 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Kagera Sugar dhidi ya
Simba Sports Club iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Juma Nyoso alituhumiwa kumpiga shabiki baada ya kumalizika
mchezo huo kinyume cha kanuni ya 36 ya ligi Kuu inayozungumzia uchezaji wa
kiungwana pamoja na Ibara 50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo imeeleza
tukio hilo la Juma Nyoso kupishana na shabiki aliyekuwa amebeba
vuvuzela na ndipo Nyoso aliposimama na kuanza kumpiga na kiatu na
kutumia goti mpaka askari wa jeshi la Polisi walipoingilia kumuokoa na
kumshikilia mchezaji huyo wakati shabiki akipatiwa huduma kwenye gari la huduma
ya kwanza.
Juma Nyoso katika utetezi wake alikana malalamiko dhidi yake
akidai kitendo alichofanya ni kukunjana na shabiki.
Kamati kupitia ripoti ya kamishna wa mchezo huo imemtia
hatiani Juma Nyoso kupitia kanuni ya 36 ya kanuni ya Ligi kuu na Ibara ya
50(1)(2) na (5) ya katiba ya TFF.
Kamati pia ilipokea taarifa za nyuma za nidhamu za Juma Nyoso
ambayo rekodi inaonesha aliwahi kufungiwa kwa makosa ya kinidhamu .
Kupitia kifungu cha 37(10)cha kanuni za ligi Kuu kamati
imemtia hatiani Juma Nyoso na imemfungia kutocheza mechi Tano(5) na faini ya
Shilingi milioni moja(1,000,000).
No comments:
Post a Comment