Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, June 27, 2017

TAIFA STARS KWENYE MTIHANI WA PILI LEO DHIDI YA ANGOLA






TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo inatarajiwa kushuka tena dimbani dhidi ya Angola katika mchezo wa pili wa kundi A wa michuano ya kirafiki iliyoandaliwa na Baraza la Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) katika Jimbo la North West, Afrika Kusini
Mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 2.30 usiku za Afrika Mashariki utafanyika kwenye uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace, Afrika Kusini.
Taifa Stars inaongoza kundi hilo kwa pointi tatu baada ya kuishinda Malawi juzi kwa mabao 2-0 katika mchezo wa awali.
Mabao ya Stars yalifungwa na Ramadhan Kichuya. Inafuatiwa na Angola yenye pointi tatu baada ya kushinda pia mchezo wa kwanza na Mauritius kwa bao 1-0.
Mchezo wa leo ni muhimu kwa kila timu kupata pointi ili kuendelea kujihakikishia nafasi ya kubaki katika michuano hiyo na hivyo kuingia hatua ya robo fainali.
Taifa Stars na Angola ni timu ambazo hazijawahi kukutana miaka ya karibuni. Hivyo, zote zinatarajiwa kucheza kwa tahadhari kutokana na kutokufahamiana.
Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alisema hali ya hewa ya Afrika Kusini ni baridi kali na inawasumbua wachezaji wake lakini amezungumza nao kuona vipi wataendelea na morali waliyoanza nayo.
“Ukweli huku kuna baridi kali lakini nimeongea na wachezaji wangu, wacheze kwa morali waliyoonyesha mwanzo, wacheze kitimu ili kupata matokeo katika mchezo ujao,” alisema Kocha kwa simu.
Baada ya mchezo wa leo, kila timu katika kundi A itakuwa imebakiza mchezo mmoja utakaochezwa kesho kutwa.
Taifa Stars itacheza dhidi ya Mauritius na Angola dhidi ya Malawi ambapo mshindi atakutana na Afrika Kusini robo fainali.
Kocha Mayanga anatumia michuano hiyo kama sehemu ya kutazama kikosi chake kwa maandalizi ya mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) dhidi ya Rwanda utakaochezwa mwezi ujao.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michez, Dk. Harrison Mwakyembe ametuma pongezi kwa Taifa Stars kwa kuichapa Malawi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Dk. Mwakyembe iliyotumwa juzi na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo, Zawadi Msalla, Waziri amewatakia Stars kila heri katika michezo inayofuata.

No comments:

Post a Comment