KOCHA wa timu ya soka ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17
‘Serengeti boys’ Bakari Shime,
amejigamba kuifunga Shelisheli katika mchezo wa kuwania nafasi ya
kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika utakaochezwa leo kuanzia saa 10.00
jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku wapinzani wakionekana kuihofia
Serengeti.
Akizungumza leo wakati wa mkutano na wandishi wa
habari, Shime alisema wamefanya maandalizi ya kutosha na kikosi chake hakina
majeruhi hivyo anawaahidi watanzania kupata burudani ya uhakika.
“Tunashukuru shirikisho limetupatia maandalizi mazuri
na kikosi hakina majeruhi hivyo naamini ushindi ni muhimu ili tuweze kujiweka
pazuri kufuzu fainali hizi”, alisema Shime.
Naye Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Shelisheli, Gavan Jeanne
ameonesha kuihofia Serengeti Boys kutokana na maandalizi ambayo wameyapata huku
akiutaja mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri ambao Serengeti ilicheza na kushinda
na safari ya India.
“Hatujawahi kushiriki michuano ya vijana, hivyo hii ni
mara yetu ya kwanza na tunajua Serengeti boys wameandaliwa vizuri kwani
wamecheza na Misri na wamefanya ziara ya kimichezo India lakini mchezo
hatutakubali kufungwa kirahisi”, alisema Jeanne.
Mchezo huu utachezeshwa na waamuzi kutoka Ethiopia,
ambao ni Belay Tadesse Asserese akisaidiwa na Tigle Gizaw Belachew na Kinfe Yilma Kinfe na
mezani atakuwepo Lemma Nigussie huku Kamishna wa akiwa Bester Kalombo.
Serengeti Boys ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016
kujiandaa na mchezo wa leo na marudiano ni
Julai 2, 2016 huko Shelisheli endapo Serengeti boys itafanikiwa kuiondoa
Shelisheli itakutana na Afrika Kusini kwenye hatua ya pili
Katika kuhakikisha hamasa inakuwepo kwa Serengeti
boys, Shirikisho la Soka nchini, jana limeiondoa kwenye hostel za Karume na
kuwapeleka kwenye hotel ya Urban Rose iliyopo katikati ya jiji.
No comments:
Post a Comment