TIMU ya
Taifa ya soka ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ kesho inashuka dimbani kucheza na Misri
ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-0 iliyopata kwenye mchezo wa awali wa
kuwania kufuzu fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika
Gabon, mwakani uliochezwa Misri.
Mchezo huu wa kundi G, utachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Taifa
Stars inahitaji ushindi ili kufufua
matumaini ya kufuzu AFCON ya mwakani wakati Misri wao sare itawafanya wafikishe
pointi nane ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye kundi lao.
Endapo
Tanzania itashinda mchezo wa leo itafikisha pointi nne kwani hadi sasa ina
pointi moja baada ya sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani huku ikibakisha mchezo wa
marudiano na Nigeria ugenini, endapo watashinda watafikisha pointi saba.
Kundi hili
baada ya kujitoa kwa Chad limebaki na timu tatu ambazo ni Misri wenye pointi
saba, Nigeria pointi nne na Tanzania yenye inashika mkia ikiwa na pointi moja lakini Misri na Nigeria
zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina faida ya mechi mbilim huu wa
leo na mwingine ni dhidi ya Nigeria utakaochezwa Septemba.
Akizungumza
na wandishi wa habari jana, kocha wa timu ya Taifa, Boniface Mkwasa alisema
mchezo wa leo ni mgumu kwani ni sawa na
fainali hivyo wanahitaji kushinda ili kujiweka pazuri kwani Misri wanakuja
wakihitaji sare.
“Wachezaji
wako vizuri, wako kwenye morali nzuri na leo (jana) tumefanya mazoezi na
wachezaji wote 26 na mimi nimefanya marekebisho kwa makosa yaliyojitokeza
kwenye mchezo dhidi ya Kenya na kinachosubiriwa ni dakika 90 tu”, alisema
Mkwasa.
Pia Mkwasa
alisema anatambua Misri ni timu nzuri kwani waliifunga Tanzania mabao 3-0 kwao
na anajua wanakuja kucheza mfumo wa kujilinda kuliko kushambulia kama ilivyo
desturi kwa timu za kiarabu lakini wao wamejiandaa kushambulia.
“Tuna deni
kubwa kwa watanzania hivyo tunajua tunatakiwa kupata matokeo mazuri ili kuwapa
faraja na kufufua matumaini ya kwenda AFCON hivyo tutashambulia sana”, alisema
Mkwasa
Mkwasa
aliwashukia watu wanaojiita wachambuzi wa soka akisema wamekuwa wakiwavunja
moyo wachezaji na kuwataka waangalie namna wanavyofanya uchambuzi kwani
wanawakatisha tamaa wachezaji na kuwaasa uchambuzi mzuri ni ule ambao unafanywa
baada ya mchezo.
No comments:
Post a Comment