ILIKUWA furaha ya aina yake kwa mashabiki wa Yanga baada ya timu hiyo kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ilikuwa huzuni kushindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara na kutoka sare ya mabao 2-2.
Mchezo huo
wa raundi ya 29 ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo hadi
mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Ndanda
ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 29 mfungaji akiwa Omari Mponda kwa njia
ya penalti baada ya Raphael Amiri kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Thabani
Kamusoko.
Hata hivyo
dakika sita baadaye Simon Msuva aliisawazishia Yanga kutokana na pasi ya
Geofrey Mwashiuya na dakika ya 40 Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la pili,
akimalizia mpira wa Haji Mwinyi.
Timu hizo
zilishambuliana kwa zamu karibu muda mwingi wa kipindi cha pili, lakini
umaliziaji ulikuwa tatizo kwa kila upande.
Wakati
mashabiki wakiamini pengine mchezo ungemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi
huo, huku furaha ikiongezeka kwa mashabiki wa klabu hiyo, mambo yalibadilika
dakika ya 79 wakati Salum Minely aliposawazisha bao hilo akimalizia kazi ya
Atupele Green na kuwafanya mashabiki wa Yanga kutulia kwa muda.
Wachezaji wa
Yanga walijipanga na kushambulia kwa nguvu kutaka kuongeza bao la tatu, lakini
Ndanda FC ilijipanga na kuhakikisha mchezo huo unamalizika kwa sare.
Furaha ya
mashabiki wa Yanga ilirejea kwa nguvu zaidi, baada ya Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Mwigulu Nchemba aliyekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo kumkabidhi
nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kombe la ubingwa wa ligi hiyo msimu
wa 2015/16.
Ni taji la
26 katika historia ya klabu hiyo kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ndiyo timu
iliyochukua taji hilo mara nyingi, ikifuatiwa na mpinzani wake wa jadi Simba
iliyotwaa ubingwa mara 18.
Yanga imekabidhiwa
kombe hilo mapema kabla ya ligi kumalizika, baada ya katikati ya wiki hii
kufikisha pointi 71 ambazo hakuna timu nyingine yoyote inaweza kuzifikia,
ambapo kwa matokeo ya jana imefikisha pointi 72.
Azam FC
inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 60 na ikishinda mechi zake mbili
zilizosalia itafikisha pointi 66, wakati Simba yenye pointi 59 ambayo leo
inacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani ina uwezo wa kufikisha
pointi 65 ikishinda mechi zake mbili zilizosalia.
Mechi
nyingine za ligi hiyo leo itakuwa kati Kagera Sugar ya Bukoba itaikaribisha
Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Uwanja wa
Mwadui Complex, Shinyanga, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City.
Prisons
itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga African Sports watakuwa wenyeji wa Azam FC.
Ligi Kuu
itamalizika Mei 21, mwaka huu, ambapo Mbeya City itacheza na Ndanda FC (Mbeya),
Coastal Union na Prisons (Tanga), Simba SC na JKT Ruvu (Dar es Salaam), Toto
Africans na Stand United (Mwanza), Azam FC na Mgambo JKT (Dar es Salaam),
Kagera Sugar na Mwadui FC (Shinyanga), Mtibwa Sugar na African Sports
(Morogoro) na Majimaji na Yanga SC (Songea).
No comments:
Post a Comment