Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba Madelu kesho
Jumamosi Mei 14, 201 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda na Young Africans katika
mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali ya Nchemba ambaye atakabidhi Kombe kwa Yanga ambao ni mabingwa
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16, wageni wengi
maalumu watakaokuwa kwenye mchezo huo ni Mkurugenzi wa Vodacom, Ian
Ferrao sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na
viongozi wengine wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi
ya Kuu Tanzania Bara (TBLB).
Mchezo huo utafanyika kwa baraka za TPLB baada ya maombi ya Young
Africans kukubaliwa na Ndanda ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo
utakaoanza saa 10:00 jioni.
Mara baada ya mchezo huo, Mabingwa Young Africans watapewa Kombe la
ubingwa, medali na fedha Sh 81,345,723; Mshindi wa Pili Sh 40,672,861;
Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 na Mshindi wa Nne atazawadiwa Sh
23,241,635.
Mchezaji Bora atapewa Sh 5,742,940 sawa na Mfungaji Bora wa Ligi na
Kipa bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom, Bia ya
Kilimanjaro, Azam, Startimes na NHIF. Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh
8,614,610 sawa na Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh
17,228,820.
Young Africans ndiyo iliyoomba kwa Ndanda kadhalika TPLB kuomba
ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa
kusafiri kwa ndege Jumapili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa
marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola utakaofanyika ama Mei 17
au 18, mwaka huu.
Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF imesema kwamba Young Africans watatumia
mchezo huo ambao Ndanda itakuwa mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara litakalotolewa na Nchemba ambaye mara nyingi
anaonekna uwanjani.
Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa,
“Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani
katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi,
utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa
katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu
kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo. Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu
za yanga ambazo Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana
kucheza mchezo huo Dar es Salaam.
Tayari Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya
hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa inacheza
mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa
taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba
inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia
nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya
msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,”
amesema Rais Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambazo
haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment