YANGA
inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kupambana na Ndanda FC katika mechi
ya duru la pili Ligi Kuu Tanzania Bara inayofikia tamati Mei 22 mwaka huu.
Yanga
inayonolewa na Mholanzi Hans Pluijm, itashuka dimbani ikiwa tayari imetetea
ubingwa wake, ikiwa inaushikilia kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo leo mchezo
huo utatumika kuikabidhi kombe lao.
Msimu
uliopita wa ligi hiyo, Yanga ilitwaa ubingwa wakiwa na mechi mbili mkononi,
lakini safari hii wamechukua wakiwa na mechi tatu.
Hiyo
inatokana na Simba kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, kitendo ambacho kiliisafishia njia Yanga kabla, kwani kulikuwa
hakuna timu ambayo ingepata pointi 69 za Yanga. Simba ingekuwa ikishinda mechi
zake zilizobaki ingefikisha pointi 67.
Lakini Yanga
iliupamba maua ubingwa huo Jumanne baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0 na
kufikisha pointi 71, ambazo hakuna timu ya kuzifikia.
Yanga
itaingia uwanjani leo, ikicheza kwa tahadhari kubwa kuhofia kupata majeruhi,
kwani Jumatano ijayo, inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Esperanca ya Angola
katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mara ya
mwisho Yanga ilipocheza na Ndanda FC, Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao
1-0, lililofungwa na beki Kelvini Yondani.
Kwa
mazingira, ni wazi Ndanda hawatokubali kupoteza mchezo wa pili mbele ya timu
hiyo, ambayo leo itakabidhiwa kombe lake la ubingwa.
Pluijm
aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kutumia mchezo wa leo kama maandalizi yake
ya mwisho kabla ya kuivaa Esperanca,
anaupa umuhimu mkubwa na wachezaji wake hawatabweteka katika mechi zote
zilizosalia.
“Sijawahi kuidharau timu yoyote inayocheza
Ligi Kuu, iwe ipo juu katika msimamo au inapigana kukwepa kushuka daraja,
nimebakiwa na mechi mbili, mfumo wangu ni ule ule wa kushambulia na kufunga
magoli mengi, kila timu nitahakikisha naifunga kwa idadi kubwa ya mabao,”
alisema Pluijm.
Kwa upande
wa kocha wa Ndanda, Abdul Mingange alisema kikosi chake ambacho ni wenyeji wa
mchezo huo watahakikisha wanapata ushindi na kujiweka vizuri zaidi. Ndanda
inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33.
Rekodi ya ubingwa Yanga
Yanga
imefanikiwa kutwaa ubingwa wa 26 mwaka huu, ubingwa ambao tangu kuanzishwa kwa
Ligi Kuu Tanzania Bara hakuna timu yoyote iliyofikia idadi hiyo.
Simba ya Dar
es Salaam yenye upinzani na Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa imetwaa mara
18.
Tambwe avunja rekodi
Mrundi Amissi
Tambwe amefunga mabao 21 hadi sasa katika ligi hiyo na kuvunja rekodi ya
Abdallah Juma aliyefunga mabao hayo 20 ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Rekodi ya
kufunga mabao mengi inashikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga
mabao 24 katika ligi hiyo mwaka 1994.
Tambwe pia
ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni nchini kufunga zaidi ya
mabao 20 katika ligi Tanzania.
Pia ameweka
rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi Ligi Kuu Tanzania Bara
ndani ya kipindi cha misimu mitatu tu baada ya kufunga mabao 54.
No comments:
Post a Comment