SIMBA kesho inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuivaa
Singida United huku ikitamba kuwapa raha mashabiki wake na kufuzu hatua ya Robo
Fainali Kombe la FA.
Kocha wa Simba, Jockson Mayanja amewataka mashabiki wa
klabu hiyo kujitokeza kwa wingi leo na kusahau matokeo ya kipigo cha mabao 2-0
walichokipata wiki iliyopita kutoka kwa Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara
kwenye uwanja huohuo.
“Tumerekebisha makosa yetu na tumedhamiria kufanya
vizuri, kila kitu kipo safi waje waone tunawapa raha,” alisema Mayanja.
Kauli kama hiyo ilizungumzwa pia na mshambuliaji Ibrahim
Ajib, aliyesema hawataki kufanya makosa na wamejipanga kuwapa furaha mashabiki
wao.
Mechi nyingine za michuano hiyo leo ni Panone FC watakuwa
wenyeji wa Azam FC kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, huku Toto Africans
wakicheza na Geita Gold Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Timu za Yanga, Ndanda FC na Coastal Union zimeshakata
tiketi ya kucheza hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
Bingwa wa Kombe hilo, ataiwakilisha Tanzania kwenye
michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mwakani, huku Ligi Kuu
Tanzania Bara bingwa wake akicheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
No comments:
Post a Comment