TIMU
ya Simba itacheza mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Sports
Club Villa ya Uganda mchezo utakaochezwa jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao ni maalum kwa
kilele cha siku ya Simba Day, ambayo hufanyika kila mwaka ikiwa na lengo la
kuwatambulisha wachezaji, benchi la ufundi na jezi awali ilikuwa wacheze na AFC
Leopards ya Kenya.
Akizungumza jijini jana Mjumbe wa kamati ya
utendaji ya Simba, Said Tuli amesema AFC Leopards ina mgogoro na wachezaji na
benchi la ufundi hivyo haitaweza kuja nchini ndio maana wakaialika Sports Club
Villa ya Uganda katika mchezo huo wa kirafiki.
“Maandalizi yapo vizuri lakini kwa bahati
mbaya au nzuri, hatutacheza tena na AFC Leopards, tutacheza na Sports Club
Villa ya Uganda ambayo inatarajiwa kuwasili leo (jana) na kufanya mazoezi katika Uwanja wa Karume”, alisema
Tuli
AFC Leopards ipo kwenye mgogoro na baadhi ya
wachezaji akiwemo kocha wao mgogoro ambao umesababisha wagome kuwepo kwenye timu hali ambayo
imesababisha Chama cha Soka cha kwao kutowaruhusu kutoka nje ya nchi hadi
wamalize tofauti zao.
No comments:
Post a Comment