WAZIRI wa
Ujenzi, John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa
michuano ya Kombe la Kagame yanayofanyika nchini kuanzia Julai 18 2015 katika
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Magufuli ambaye
ameteuliwa kuwa mgombea wa Urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni baada ya kufungua rasmi michuano
hiyo, atashuhudia mechi itakayokutanisha miamba ya Afrika Mashariki timu ya
Yanga dhidi ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya.
Akizungumza
na wandishi wa habari Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Baraka
Kizuguto alisema kuwa taratibu zote zimekamiliki na timu zitaanza kuwasili
kesho wakati waamuzi wanaanza kuwasili leo.
“Waamuzi wa
michezo hiyo wanatarajiwa kuwasili kesho (leo) sambamba na kamati ya ufundi kwa
ajili ya mitihani ya utimamu wa mwili (Physical Test) itakayofanyika siku ya
alhamisi, na kamati ya ufundi watakua wakikagua viwanja na kuweka vipimo kabla
ya ufunguzi rasmi wa michuano hiyo”, alisema Kizuguto
Michuano ya
Kagame inatarajiwa kuanza kutimua vumbi siku ya jumamosi kwa michezo mitatu,
ukindoa mechi ya Yanga na Gor Mahia, mechi zingine zitakua ni kati ya APR dhidi
ya Al Shandy uwanja wa Taifamchezo utakaochezwa
saa 8 mchana wakati KMKM na Telecom zitacheza uwanja wa Karume saa 10
jioni.
Yanga
inayofundishwa na Hans van Pluijm imewahi kutwaa ubingwa mara tano (Mwaka 1975,
1993, 1999, 2011, na 2012) wa michuano hiyo watakuwa na kazi moja tu ya
kujaribu kuifikia rekodi ya Simba, inayoongoza kutwaa Kombe hilo mara nyingi,
ikiwa imeweza kufanya hivyo, mara sita.
Pia Yanga
imemaliza kama washindi wa pili mara mbili, mwaka 1976 ilipofungwa na Gor Mahia
2-1 jijini Kampala na mwaka 1992 ilipolala kwa mikwaju ya penati mbele ya
watani wao wa jadi, Simba.
Gor Mahia ambayo
inafunzwa na kocha Frank Nuttal, raia wa Uskochi mara ya mwisho kutwaa ubingwa
wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1985, lakini imetwaa ubingwa huo mara 5
(1976, 1977, 1980, 1981, 1985) hivyo kama ilivyo Yanga wana kazi ya kuakikisha wanavunja rekodi ya Simba ambayo mwaka huu haishiriki.
Mchezo wa
ufunguzi kati ya Yanga dhidi ya Gor Mahia unaonekana kuteka hisia za
wapenzi wa soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kwani ni takribani miaka 19
timu hizo mbili haziwaji kukutana katika ardhi ya Tanzania.
Gor
Mahia na Yanga zipo kwenye kundi A pamoja na timu za Al Khartoum ya Sudan, KMKM
ya Zanzibar na Telecom ya Djibout.
No comments:
Post a Comment