PAZIA la Ligi Kuu ya Tanzania Bara limehitimishwa leo kwenye viwanja
saba tofauti na kushuhudiwa timu mbili
zinazomilikiwa na majeshi Ruvu Shooting na Polisi Moro zikishuka daraja.
Ruvu inayonolewa na kocha, Tom Olaba ilikuwa ugenini Uwanja wa Kambarage
mkoani Shinyanga na kujikuta ikipokea kipigo cha bao 1-0 na wenyeji wao Stand
United ambayo ushindi huo umeifanya kufikisha pointi 31 katika nafasi ya 10.
Polisi Moro iliyopanda kucheza Ligi Kuu msimu huu, ilikubali kipigo cha
bao 1-0 kutoka kwa Mbeya City na kujikuta ikirudi ilipotoka na hiyo inatokana
na mwenendo wa kusuasua tangu kuanza kwa msimu huu ikiwemo uongozi kubadilisha
makocha mara kwa mara.
Polisi Moro ndiyo timu pekee msimu huu ambayo imefundishwa na makocha
watatu, ilianza na Adolfu Rishald kisha ikamfukuza na kumchukua Amri Said,
ambaye naye aliamua kujiondoa na nafasi yake kuchukuliwa na John Tamba, lakini
hadi siku jana walijikuta wakiburuza mkia wakiwa na pointi zao 25 katika mechi
26 walizocheza.
Katika uwanja wa Nang'wanda Sijaona mkoani Mtwara, Mabingwa wapya wa
msimu huu Yanga waliendelea kuonja shubiri baada ya kupoteza mchezo huo kwa
kufungwa bao 1-0 na wenyeji Ndanda FC, Wakati kwenye Uwanja wa Azam Complex
wenyeji Azam walitoka sare ya bila kufungana na Mgambo JKT ya Tanga.
Kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kocha, Mbwana Makatta,
alifanikiwa kuiokoa timu ya Tanzania Prisons isishuke daraja msimu huu baada ya
kuilazimisha sare ya bila kufungana na Kagera Sugar aliyomaliza nafasi ya sita
ikiwa na pointi 32, huku sare hiyo ikiwasaidia maafande hao kufikisha pointi 29
na kuepuka janga la kurudi kushuka daraja la kwanza msimu ujao.
Katika uwanja wa Manungu Turiani, Mtibwa Sugar ililala nyumbani kwa
kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union ya Tanga na matokeo hayo kuifanya timu hiyo
iliyokuwa na kipindi kigumu licha ya kunza msimu huu vizuri kumaliza nafasi ya
saba msimu huu ikiwa na pointi 31 huku Wagosi wa Kaya wakimaliza nafasi ya tano
wakiwa na pointi 34.
No comments:
Post a Comment