MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Katibu Mkuu wa zamani wa klabu ya
Simba, Hassani Othman ‘Hasanoo’ na wenzake wawili baada ya upande wa mashitaka
kushindwa kuthibitisha mashitaka ya wizi wa Shaba za Sh milioni 400.
Hata hivyo baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo
Hassanoo alirudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu
uchumi.
Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakama hapo na
Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, baada ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka aliyetakiwa
kusoma hukumu hiyo kutokuwepo.
Hakimu Fimbo alisema katika ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo na mashahidi 13 wa upande wa mashitaka haujathibitisha kuwa
washitakiwa hao walikula njama au kuwasiliana kwa kupanga kutenda kosa hilo kwa
njia yoyote.
Aidha alisema hakuna shahidi aliyethibitisha
kuwa madini hayo yaliibiwa na awali upande wa mashitaka ulileta washitakiwa wanne na baadaye
mmoja kuondolewa, lakini ilishangaza kuona mtu huyo hakuitwa mahakamani kutoa
ushahidi.
Katika mashitaka ya kupatikana na mali
iliyoibiwa, Hakimu Fimbo alisema hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa washitakiwa
hao waliiba au kupokea shaba hizo.
"Kulingana na ushahidi uliotolewa
mahakamani, washitakiwa hawana hatia na wote nawaachia huru," alisema
Hakimu Fimbo.
Mbali na Hassanoo, washitakiwa wengine ni
Wambura Mahenga ambaye ni mshitakiwa wa kwanza na Dk Najim Msenga ambaye ni
mfanyabiashara maarufu wa madini na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi taifa (NEC).
Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa
matatu, ambapo wanadaiwa Agosti 26, mwaka huu walikula njama ya kutenda
kosa la kuiba vitu vilivyokuwa vikisafirishwa.
Kosa la pili ilidaiwa mahakamani hapo kuwa,
washtakiwa hao waliiba shaba hiyo mali ya Kampuni ya Libert Express(T)Limited
iliyokuwa ikisafirishwa na lori T 821 ABC lililokuwa na tela T 566 BCZ
likitokea Zambia.
Katika kosa la tatu ilidaiwa kuwa, watuhumiwa
hao walipokea shaba hizo huku wakijua kuwa, mali hizo zimepatikana
kwa njia isiyo halali.
Akizungumza nje ya Mahakama baada ya kutolewa
kwa hukumu hiyo, Dk Msenga alisema kuwa hukumu hiyo imetolewa kwa kuzingati
haki, kutokana na ukweli ulioelezwa mahakamani hapo.
No comments:
Post a Comment