Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, August 1, 2013

WAKALI 10 WA KUCHATI TWITTER, CRISTIANO, KAKA, NEIYMAR

KUANZISHWA kwa mitandao ya kijamii, imesaidia sana kurahisisha mawasiliano, zaidi hata simu za kiganjani sifanyavyo. Kuna uwezekano kwa sasa nchi hii ikawa nambari moja kwa mawasiliano, ikilinganishwa na njia nyingine yoyote. Kama wewe huna akaunti katika moja ya mitandao wa kijamii kati ya Myspace, Facebook, Twitter, Whatsapp ana Veepiz, jua umeachwa nyuma.

Ilianza Myspace iliyokuwa ya wachache sana - ilikuwa ya wale wanaojua maana ya internet, baadaye Mark Zuckerberg akaanzisha Facebook, ambayo imekamata dunia kwa sasa. Lakini mpinzani mkubwa wa Facebook ni Twitter, ambao hakika umetikisa zaidi ya Facebook kutokana na idadi ya wateja.
Hata hivyo, ukurasa wa Twitter umevamiwa zaidi na wanasoka mastaa kwa kuwa na wafuasi wengi kama ilivyoripotiwa na tovuti ya bleacher.com. Ifuatayo ni orodha ya wachezaji wa soka wanaotisha kwenye mitandao hii.

1. Cristiano Ronaldo (Real Madrid)

Huyu ndiye kinara kwa wanasoka kwa kuwa na marafiki wengi kwenye mtandao wa twitter. RC7 kama anavyojiita ana jumla ya mashabiki (followers) milioni 19.9 na huenda wamefikia milioni 20 mpaka makala haya unayasoma. Kila kukicha idadi ya mashabiki inaongezeka.
Anapendwa kuanzia uwanjani, mambo fulani ya ndani hadi kwenye mtandao. Miguu ya ukakamavu, mbio, ufungaji mabao, staili ya uchezaji, kipaji cha kupiga mipira iliyokufa na penalti, sura yenye mvuto ni sababu zinazomfanya CR7 kupendwa na wadau na wasiokuwa wadau wa soka.
Ukweli tangu ajiunge na Real Madrid kwa uhamisho iliovunja rekodi, pauni milioni 80 miaka minne iliyopita, tayari ameingia kwenye orodha ya wanasoka walioifungia Real mabao mengi, mabao 146 katika michezo 135.  hali inayomuongezea umaarufu ndani na nje ya uwanja hasa wa akina dada.
Usije ukachanganya mahesabu haya. CR7 anaoongoza kwa upande wa wanasoka tu, lakini anafyata mkia kwa msanii dogo Justin Bieber, ambaye ndiye anaongoza kwa watu wengi kwa ujumla.

2. Kaka (Real Madrid)

Japo soka la Real limemuangusha tangu ajiunge nao miaka mitano iliyopita, lakini Kaka anabaki kuwa mmoja wa wanasoka wanaopendwa zaidi katika sayari hii.
Ana jumla ya watu milioni 16.1 kwenye ukurasa wake wa Twitter, na amekuwa akitumia muda mwingi wa usiku kuchati, na wala hana presha ya kutupiwa virago kwani anajua uongozi wa Real haumpendi.
Inasemekana idadi ya wafuasi/mashabiki wake ni watu wa dini zaidi ambao wamekuwa waki-‘post’ ujumbe wa kumuombea abaki Bernabeu. Kaka amekuwa akiwavuta mashabiki kwa kuandika kwa lugha tatu - za Kihispania, Kireno na Kiingereza, hivyo kutega kila anga.
Maombi hayo yanaweza kusikilizwa baada ya ujio wa Carlo Ancelotti kama kocha mpya wa Real, aliyemfundisha miaka mitano iliyopita pale AC Milan. Ancelotti ndiye alimsajili na kumfanya kuwa mchezaji bora wa dunia 2007, kabla ya kuondoka msimu wa 2008, ujio wa kocha huyo, huenda Kaka akarejeshewa namba.
Baada ya mchezo dhidi ya Bournemouth wiki iliyopita, Kaka alituma picha za mchezo huo kwenye twitter kuashiria amerudi tena.

3. Neymar da Silva Jr (Barcelona)

Anatazamiwa kuwa nyota mpya wa Barcelona. Tovuti ya kibiashara ya ‘per Eurosport-Yahoo’ ilimtaja Neymar kama mchezaji anayeongoza katika matangazo ya kibiashara.
Lakini nyota huyo amekuwa miongoni mwa wanasoka wenye mashabiki wengi katika mtandano wa kijamii wa twitter, akiwa na jumla ya watu milioni 7.5.
Wakati akiwaaga mashabiki wa Santos kupitia mtandao wa kijamii, idadi iliongezeka, hali iliyosababisha mtandao kuwa ‘bize’ na kushindwa kufanya kazi.
 4. Ronaldo Moreira ‘Ronaldinho’ (Atletico Mineiro)
Pamoja kwamba siku za umaarufu wake zimekwisha, tofauti na alivyokuwa AC Milan na Barcelona, lakini bado mashabiki wanamkumbuka.
Umaarufu wake umeonekana kupungua tangu alipoamua kucheza soka la nyumbani katika klabu ya Flamengo msimu wa 2011, kabla ya kujiunga na Atletico Mineiro ambapo nacheza mpaka sasa.
Lakini hata hiyo haitoshi mashabiki kumsahau mkali wao na hivi karibuni imeripotiwa ana jumla ya watu milioni 6.76 kwenye Twitter na kuwapiku Wayne Rooney na Andres Iniesta.

5. Wayne Rooney (Manchester United)

Wayne Rooney ‘Wazza’ ndiye kinara wa wachezaji wa Kiingereza, akiwa nafasi ya tano. Akaunti yake muda wote iko bize na stori lukuki kutokana na wingi wa marafiki, jambo ambalo linampa wakati mgumu hata yeye. Ana jumla ya marafiki milioni 6.75.
Kubadilisha habari za wasifu wake ‘profile’ kwa kuondoa neno la ‘mchezaji wa Manchester United’ alizua mjadala usio na mwisho, huku marafiki wakiongezeka kila kukicha kuchangia mada iliyopo ya kuondoa neno hilo, na kuhisiwa anaweza kuondoka United, kwa mujibu wa gazeti la Guardian.
Rooney, hajachangia zaidi ya kuwa bize na ku-post picha mbalimbali pamoja na kuhariri wadhamini wa ukurasa wake.

6. Andres Iniesta (Barcelona)

Kuna mchezaji anayependwa kwa sasa zaidi ya huyu jamaa? Hakuna, lakini tunapokuja kwenye mitandao, hafui dafu, maana anashika nambari sita.
Iniesta anamzidi mchezaji mwenzake, Gerard Pique marafiki 800,000, idadi inayomfanya kuwa Mhispania wa kwanza kwenye orodha hii.
Uwezo binafsi, chenga za maudhi, ukakamavu na pasi murua zenye macho, zinamfanya Iniesta kupendwa na rika zote.
Idadi ingeongezeka maradufu, lakini tatizo huwa anatuma jumbe kwa lugha ya Kihispania, hali inayowanyima nafasi wasiojua lugha hiyo. Lakini kuonesha kuwa wako naye, hawaachi kuweka maoni yao kwenye picha anazotuma, hasa pindi Barca inapopata ushindi.

7. Gerard Pique (Barcelona)

Ni machungu juu ya machungu, wakati akifuta machozi ya kushindwa kutwaa ubingwa wa mabara, leo hii analia na kuondoka gafla kwa aliyekuwa kocha wake pale Barcelona,  Tito Vilanova. Baada ya Hispania kufungwa 3-0 na mabingwa wapya wa kombe hilo, Pique aliandika kwenye twitter jinsi alivyoumizwa na mchezo huo, mashabiki walimpoza, ingawa sidhani kama kweli alipozwa na marafiki hao zaidi ya ‘toto la Kikolombia’ Shakira aliye na haki ya kumpoza kwa kila uchungu. Leo hii Pique, ana jumla ya marafiki milioni 6.37 kwenye Twitter.

8. Francesc Fabregas (Barcelona)

Suala la kuhisishwa kujiunga na Manchester United, hivi karibuni, huenda limechangia kiasi kikubwa kuongezeka kwa wafuasi kwenye akaunti yake ya Twitter. David Moyes ametoa ofa mpya ya pauni mil. 30 kwa nahodha huyo wa zamani wa Arsenal, the Telegraph, limeripoti.
Lakini nyota huyo (26), ambaye huandika kwa lugha ya Kiingereza, Kihispania pamoja na ki- Catalan, amezidi kuufanya mtandao kuwa bize kwa wingi wa watu.
Fabregas, ana watu wanaofikia mil. 5.38, wanaofuatilia ‘post’ zake juu ya kurejea tena Ligi Kuu England. Hata hivyo, amekuwa akipendelea ku-post mabao yanayohusu familia yake kwa kuweka picha za dada yake pamoja na wachezaji wenzake wa Barca, tofauti na marafiki wanachosubiria.

9. Carles Puyol (Barcelona)

Vyombo vya habari vya Hispania vimeendelea kumuandama Carles Puyol kwa kumtafutia mbadala Camp Nou. Na vimekuwa vikimshawishi beki wa Chelsea, David Luiz, kuchukua nafasi hiyo, gazeti la Mirror linaripoti.
Lakini Puyol, katika kupingana navyo, amezidi kuweka picha akiwa na nyota wengine wa Barca na kuwaeleza yuko fiti na msimu ujao. Picha hizo zimewavuta marafiki kwenye akaunti yake na kufikia milioni 5.

10. Rio Ferdinand (Manchester United)

Ni Mwingereza wa pili, baada ya Rooney kung’ara katika anga za mawasiliano ya kidijitali. Mbali na wingi wa marafiki, pia akaunti yake anaitumia kama njia ya kutangazia biashara pamoja na kuuza picha na majarida kadha wa kadha. Kupitia biashara zake, Ferdinand ana idadi inayofikia mil. 4.5 kwenye akaunti yake.
Hata hivyo, akaunti yake inaweza kuwa si lolote kutokana na adhabu za hapa na pale alizokumbana nazo kwa kuandika ujumbe usiotakiwa. Si mara moja Ferdinand kuadhibiwa kwa kulipa faini, ikiwemo ya kumkejeli beki wa Chelsea, Ashley Cole na katika sakata la John Terry la ubaguzi.

Wengi watajiuliza, mbona mchezaji bora wa dunia na kipenzi cha wengi, Lionel Messi amesahaulika? Hapana, hajasahaulika. Messi hana marafiki, kulinganisha na mastaa hawa, huku akiwa na watu milioni 1.64.

No comments:

Post a Comment