Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, July 24, 2013

WENGER ANAWALISHA 'MATANGO PORI' WADAU WA HIGUAIN

LONDON, England

GONZALO Higuain, Wayne Rooney, Edinson Cavani, Gareth Bale, Luis Suarez, pengine na Cristiano Ronaldo, ni majina yaliyotikisa katika usajili msimu huu.

Hata hivyo, ni Cavani tu amekata mzizi wa fitina kwa kusaini Paris Saint Germain PSG ya Ufaransa, wakati wengine ukibaki usajili wa porojo.

Yote tisa, kumi ni sakata la mshambuliaji wa Real Madrid, Gonzalo Higuain kujiunga na Arsenal, sakata linaloingia mwezi wa tatu sasa, bila kukamilika.

Zimebaki kuwa kelele za kisiasa, tofauti na kauli aliyotoa kocha Arsene Wenger, mwishoni mwa msimu uliopita. Aliapa kuachana na wachezaji wa bei poa, zaidi msimu huu angefanya usajili wa mastaa ambao watafuta ukame wa miaka nane bila kombe.

Higuan amekuwa gumzo msimu mzima, hata hivyo mashabiki wa Arsenal wamekuwa wavumilivu kwa hilo. Wenger alianza ‘siasa’ hizo kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu uliopita kwa kutuma ofa, mpaka leo hii biashara hiyo imeingiliwa na vigogo vya Chelsea na Napoli.

Inasemekana hii leo mchezaji huyo yupo njiani kutua Napoli, baada ya makubaliano ya kiasi cha Euro milioni 35, kwa mujibu wa gazeti la Corriere dello Sport la Italia. Habari mbaya kwa wana-Arsenal.

Fuatilia usajili wa Higuain tangu Wenger atangaze kumng’oa Bernabeu mpaka leo inadaiwa kujiunga na Napoli.

Mei 14: Arsenal watuma ofa ya pauni mil. 22

Katikati ya Mei, Wenger aliamua kumgeukia Higuain, baada ya kuona kuna dalili ya kumkosa mchezaji aliyekuwa akimuwinda kwa muda mrefu, Stevan Jovetic wa Fiorentina.
Hii leo Jovetic yupo viunga vya jiji la Manchester kwenye kikosi cha Man City, baada ya Arsenal kukataa kukamilisha dau la pauni milioni 25 walizotaka Fiorentina, kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail.
Kufa kwa dili la Jovetic, Wenger alimgeukia Higuain kama ‘plan B’. Lakini alionekana kutokuwa ‘serious’ na usajili huo, kwani tayari kocha wa Madrid kipindi hicho, Jose Mourinho alimuweka sokoni kwa bei poa-pauni mil. 22, Arsenal walibaki na kauli za subiri kidogo.

Mei 20: Watangaza ofa pauni mil.19

Kufuatia udhamini wa jezi kutoka kwa kampuni ya Puma, udhamini wa uwanja pamoja na mkwara wa Stan Kroenke kumwaga mamilioni kuijenga Arsenal, siku hiyo hiyo waliweka mezani pauni mil. 19 kumpeleka Emirates.
Hiyo iliendana na falsafa ya kocha Wenger aliyoahidi mwishoni mwa msimu uliopita. Wadau walisapoti ujio wa nyota huyo raia wa Argentina, lakini zimebaki kauli zile zile.

Juni 7: Arsenal waapa kumsajili Higuain

Ilikuwa habari njema kwa mashabiki wa Arsenal, baada ya Real Madrid kutangaza kuwa tayari kumuuza nyota huyo majira haya. Ni Arsenal tu ilikuwa imetuma ofa ya kumsajili, kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph.
Madrid walitaka pauni mil.22, kiasi alichokitaja Wenger hapo awali, lakini wakati huu profesa alishikwa na kigugumizi, zaidi alisema alikuwa na thamani si zaidi ya pauni mil. 20.
Sita-sita yake, imemfanya kushtukia Higuain anafikia thamani ya pauni mil. 37 hii leo.

Julai 4: Arsenal kumlipa pauni 100,000 kwa wiki

Uvumi ulioje? Kuwa Wenger alifikia makubaliano na Madrid kumsajili kwa kiasi cha pauni mil. 23 pamoja na kutangaza kumpa mkataba wa miaka mitatu na mshahara wa pauni lakini moja, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian. Mshahara huo ungemfanya kuwa wa pili nyuma ya Lukas Podolski anayepata pauni 107, 000 kwa wiki.
Mashabiki walisubiri kumuona Higuain ndani ya uzi mwekundu ama njano, ndoto wanayoiota mpaka sasa. Chuki ya mashabiki ilichochewa na kauli ya mchezaji mwenyewe, ya; “Nimekuwa Bernabeu miaka saba, ni muda wa kubadilisha mazingira. Nataka niende sehemu ambayo kweli watanithamini na wananipenda,” alisema Higuain.
Kauli hiyo, ni kama iliwaita Juventus, licha ya kumsajili Tevez kwa pauni mil.10, lakini walitangaza nia ya kuwania saini ya Higuain, hali iliyowachefua The Gunners kuingiliwa kibiashara.

Julai 8: Real Madrid-hakuna ofa ya Arsenal

Ilikuwa kama kuwalisha matango pori au danganya toto ya Wenger, ambaye siku nne alitangaza kumalizana na uongozi wa Madrid. Mashabiki walianza kukata tamaa na kauli za kocha wao tangu Mei.
Julai 8, Rais wa Madrid, Florentino Perez, aliwapa ukweli mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kusema kuwa hajapokea ofa yoyote kutoka kwa Wenger, alisema mpaka tarehe hiyo, Madrid walighairi kumuuza.
“Hatutaki tena kumuuza, tumeona umuhimu wake na ataendelea kuwa nasi,” alisema Perez kwa mujibu wa gazeti la the Mirror.

Julai 11: Arsenal kuchukua 3 kwa mpigo

Alikuja na sera mpya ya kuwataka nyota Luis Suarez (Liverpool), Wayne Rooney (Man United) pamoja na Higuain mwenyewe.
Daily Stars, waliripoti kuwa Kocha Wenger alisema alikaa na uongozi wa timu yake na kumtaka kusajili nyota wengine wawili.
Ilileta wasiwasi kidogo, kwani walikuwa wanafanya usajili wa maana, huku wakiwa na kumbukumbu ya kuangamiza mil.15 kwa Andrei Arshavin, ambaye hakufanya la maana, licha ya kuwa mmoja wa wachezaji mastaa.

Julai 15: Ni Suarez, Higuain tu!

Gazeti la London Evening Standard, liliripoti kuwa Gonzalo Higuain Julai 15 alikuwa na maongezi na kocha wake mpya, Carlo Ancelotti, huku mashabiki wa Arsenal wakijipa moyo alikwenda kumuomba kuuzwa.
Jasho liliendelea kuwatoka Arsenal, kwani ndiye lilikuwa jicho lao usajili wa mwaka huu, huku wakimtaja Luis Suarez kusaidiana naye katika safu ya ushambuliaji.
The Gunners waliapa kuvunja rekodi kwa kumsajili Suarez kwa pauni mil. 35, baada ya kubembeleza Madrid kumuachia Higuain.
 Julai 17: Higuain kumrithi Cavani Napoli,
Matajiri wa Qatar - ambao ni wamiliki wa Napoli, walimtaja Higuain kama mrithi pekee wa Edinson Cavani, aliyekuwa ametimkia PSG Julai 16.
Jeuri la pauni mil. 100 walizonazo Napoli msimu huu, zilitibua biashara ya Wenger kwa Higuain, huku Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis akikiri kumalizana na mchezaji.
“Ni kweli tumekuwa na mazungumzo Higuain na mchezaji mwingine, Leandro Damiao wa Brazil. Fedeha za Cavani (euro mil. 64.5) kuongeza na euro mil.60 tulizokuwa nazo, zinatufanya kuijenga Napoli.

Julai 18: Higuain: Chelsea watapiku Arsenal

Gazeti la the Mirror, Julai 18, liliripoti kuwa chanzo cha karibu cha Higuain kilidai kuwa klabu ya Chelsea ilikuwa na nafasi kubwa ya kumpata baada ya Arsenal kutoonesha nia ya dhati. "Mourinho ananitaka pale Chelsea. Wengine wanababaisha,” kilibainisha chanzo hicho.

Julai 21: Arsenal warudi kwenye mbio

Kitendo cha Napoli kusita kutoa pauni mil. 35 wakati Madrid wanajua wanazo kutokana na mauzo ya Edinson Cavani, kiliwapa ahueni ya Arsenal kurudi kwenye mbio za kutaka saini ya Higuain.
Awali walionekana kukata tamaa, kwa kuingiliwa na vigogo, lakini wametupa kete yao tena kuhakikisha wanampata. Wana matumani baada ya mchezaji mwenyewe kudai hapendwi Bernabeu. 
Gazeti la the Independent, linaripoti kuwa Arsenal wako tayari kuongeza ofa, kufuatia Napoli kukagomea kutoa zaidi mil. 35.

Imebaki kuwa siasa ama wasemavyo mashabiki kulishwa ‘matango pori’ na muda wowote anaweza kutua klabu nyingine, wakati mashabiki wakiwa wameandaa sherehe zao huko Emirates.

No comments:

Post a Comment